Home Mchanganyiko SERUKUMBA ATOA RAI KWA CHUO CHA ATC KUTANGAZA PROGRAMU ZINAZOTOLEWA NA CHUO...

SERUKUMBA ATOA RAI KWA CHUO CHA ATC KUTANGAZA PROGRAMU ZINAZOTOLEWA NA CHUO HICHO

0

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Peter Serukamba akiwa kwenye picha ya Pamoja na Mawaziri wanaoshugulikia Elimu na wajumbe wa Kamati hiyo mara baada ya kukagua miradi ya Elimu inayotekelezwa Chuo cha Ufundi Arusha

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo wakiangalia kwa furaha namna mwanafunzi wa Chuo cha Ufundi Arusha anavyotumia mashine za kujifunzia wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilipotembelea ATC.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ikipata maelezo ya vifaa vinavyotumika kwenye karakana ya ufundi Magari wakati waliotembelea Chuo cha Ufundi Arusha (ATC).

Mmoja wa wakufunzi wa Chuo cha Ufundi Arusha akionesha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii namna wanavyotumia vifaa vya kisasa vilivyopo chuoni hapo wakati wa kufundisha.

********************************

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Peter Serukamba ametoa rai kwa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kutangaza programu na huduma ziazotolewa Chuoni hapo ili wananchi wanufaike na huduma hizo.

Serukamba ametoa rai hiyo Jijini Arusha wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilipotembelea chuo cha Ufundi Arusha kukagua miradi ya elimu inayotekelezwa chuoni hapo.

“Nimefurahishwa na ubora wa huduma na wanafunzi wa chuo hiki sasa wakati umefika kwa chuo kujitangaza ili kupata masoko ya bidhaa zinazozalishwa lakini pia kuongeza wanafunzi wengi zaidi kujiunga na kozi zinazofundishwa hapa” amesema Serukamba.

Pia amekitaka Chuo hicho kuanzisha Kampuni itakayosimamia na kufanya kazi mbalimbali kibiashara katika maeneo waliyobobea ikiwemo uhandisi ujenzi, ufundi wa magari, umeme na maeneo mengine, hatua ambayo itasaidia kukuza mapato ya ndani ya Chuo ambayo yatakiwezesha kutekeleza miradi mingine ya kimkakati.

Mheshimiwa Serukamba amesema Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa Miradi ya Serikali ambayo Chuo cha ATC kinasimamia na kukitaka chuo hicho kupanua wigo wa wateja kwa kutafuta miradi toka sekta Binafsi ili kuondoa utegemezi wa Miradi ya Serikali pekee.

Aidha, Mheshimiwa Serukamba ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika wa miundo mbinu ya kufundishia katika chuo hicho ikiwa ni pamoja na kukipatia kazi za usimamizi wa Miradi ya Ujenzi katika Vyuo vya Ufundi na Ualimu.

Pia amekipongeza Chuo cha Ufundi Arusha kwa kuendesha programmu ya Mafunzo ya muda mfupi ya ufundi ujenzi ambayo mpaka sasa takriban wanafunzi 305 wamehitimu mafunzo hayo, huku akiishauri Wizara ya Elimu, kushirikiniana na Chuo hicho kuhakikisha wahitimu hao wanapata nafasi ya kufanya kazi katika miradi ya ujenzi inayoendelea.

Nae Mbunge wa Biharamulo Magharibi na Mjumbe Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Oscar Mukasa amesema kwa mara ya kwanza ameona chuo kimesimama katika dhamira yake, na hivyo kupongeza hatua ya Chuo cha ATC kujikita katika kutoa mafunzo kwa ubora ambayo ndio msingi wa kuanzishwa kwake, akiongeza kuwa vipo vyuo ambavyo vilianzishwa kwa malengo fulani lakini kwa sasa vinatekeleza malengo mengine.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwenye elimu ya Ufundi kwa kuimarisha vyuo vya ufundi wa kati na ufundi stadi kwani ndiko wataalamu wanapopatikana wa kufanya kazi kwenye viwanda na ndio maana serikali imewekeza takriban sh bilioni 16 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na mitambo ya karakana zote za chuo hicho.

“Tangu serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani viwanda 800 vimeanziswa, hii maana yake ni kwamba tunahitaji kuzalisha vijana wengi wenye ujuzi wa kufanya kazi katika viwanda hivyo,” amesema Profesa Ndalichako

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Ufundi Arusha Prof. Siza Tumbo amesema katika uongozi wake atahakikisha chuo hicho kinajitangaza kwa kupitia njia anuahi za mawasiliano ili huduma zinazotolewa chuoni hapo ziwafikie watanzania wengi zaidi, ikiwa ni pamoja na kuwa na mkakati wa kuongeza idadi ya wasichana kujiunga na chuo hicho.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha Dkt Musa Chacha amesema kwa sasa Chuo kina mipango mingi ikiwa ni pamoja na kujenga bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 500, kuongeza mapato ya ndani kutumia kazi zinazofanyika, kuendeleza kituo cha mafunzo ya nishati jadidifu cha Kikuletwa na kituo cha mafunzo ya kilimo na umwagiliaji cha Oljoro pamoja na ukarabati wa miundombinu ya Chuo.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii iko Mkoani Arusha katika ziara ya kukagua miradi ya Elimu inayotekelezwa katika Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo Kikuu cha Nelson Mandela.