Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Dkt. Jasson Rweikiza (Mb), akitazama ramani ya kiwanja cha Mungumaji ambacho Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Singida kinatarajiwa kujengwa wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua kiwanja hicho iliyofanyika jana.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, wakisikiliza maelezo ya mpango wa ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Singida kutoka kwa Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma na Mtendaji Mkuu wa Taasisi, Dkt. Selemani Shindika, wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua kiwanja hicho iliyofanyika jana.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb) akifafanua kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, uvumi ulioenea wa Serikali kukihamishia Dodoma Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Singida wakati wa ziara ya kamati hiyo iliyofanyika jana ya kukagua kiwanja cha Mungumaji ambacho Kampasi ya Singida inatarajiwa kujengwa.
Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Selemani Shindika akitoa ufafanuzi kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, kuhusu kiwanja kilichonunuliwa kwa ajili ya Ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Singida wakati wa ziara ya kamati hiyo iliyofanyika jana.
***************************
James Mwanamyoto – Singida
Tarehe 14 Machi, 2020
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb), amekanusha uvumi ulioenea kuhusiana na Serikali kukihamishia Dodoma, Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Singida.
Mhe. Mkuchika amekanusha uvumi huo jana kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua kiwanja cha Mungumaji ambacho Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Singida kinatarajiwa kujengwa.
“Chuo kimenunua kiwanja hicho kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi ya Singida, hivyo nashangazwa na uvumi wa kukihamishia Dodoma, na kuongeza kuwa iwapo Serikali
ingekuwa na lengo la kuhamisha Kampasi hiyo, isingeingia gharama ya kununua kiwanja Singida,” Mhe. Mkuchika amefafanua.
Mhe. Mkuchika amesema kuwa, Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kina Kampasi sita za kikanda katika mikoa ya Singida, Tabora, Mbeya, Tanga, Dar es Salaam na
Mtwara, hivyo kinachofanyika hivi sasa ni kununua viwanja kwa ajili ya kuwa na majengo yake na kuondokana na gharama kubwa ya kupanga katika majengo ya watu
binafsi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Dkt. Jasson Rweikiza (Mb), amekipongeza Chuo cha Utumishi wa
Umma baada ya Kamati kuridhishwa na kiwanja kilichoandaliwa kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi ya Singida ikiwa ni pamoja na jitihada za chuo kutenga fedha za ndani shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Aidha, Mhe. Rweikiza ameishauri Menejimenti ya Chuo kuomba fedha Serikalini ili kuharakisha ujenzi wa Kampasi hiyo kutokana na umuhimu wa Chuo hicho kwa Watumishi wa Umma na wananchi.
Akitoa maelezo kuhusu kiwanja kilichotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi ya Singida, Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Selemani Shindika, amesema kiwanja hicho kina ukubwa wa ekari 76.
Dkt. Shindika ameongeza kuwa, kiwanja hicho kimenunuliwa ili Chuo kiweze kumiliki majengo yake, kwani Kampasi hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011 imekuwa ikitumia majengo ya kukodi kwa mtu binafsi ambayo gharama yake ni kubwa sana.