Na Magreth Mbinga
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kwa asilimia tisini katika vita ya kupambana na dawa za kulevya kutokana na kufanya marekebisho makubwa ya kisheria kwa kutunga sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.
Hayo yamezungumzwa na kamishna msaidizi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya James Kaji kwenye mazungumzo yake na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.
Pia alisema katika mkutano wa 63 wa kamisheni ya Kimataifa ya kudhibiti Dawa za kulevya duniani (CND 63) uliofanyika Viena Australia , mkuu wa Shirika la umoja wa Mataifa linaloshughulikia Dawa za kulevya na uhalifu (UNODC) Bi Ghada Fathi Wally amesema “Tanzania ni moja kati ya nchi chache barani Afrika zilizofanikiwa kupunguza madhara yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya.
Sanjari na hayo Kaji amesema pamoja na mafanikio makubwa kwa masikitiko makubwa baadhi ya magazeti wanaichafua nchi ya Tanzania kwa kuandika habari zisizo sahihi kuhusu udhibiti na mapambano dhidi ya dawa za kulevya.”Kitaifa nchi yetu imekuwa ya mfano wa kuigwa kwani hata nchi za Uganda ,Msumbiji ,Ghana na Norway zimeomba kujifunza kutoka kwetu mfumo wa utendaji kazi wetu pamoja na sheria yetu inayofanya kazi” amesema Kaji.
Vilevile aliwataka waandishi wa habari kuwa makini katika shughuli zao za uandishi na kutumia vema vyanzo vya uhakika na kuzingatia maadili ya uandishi.
“Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya kwa mujibu wa sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya kifungu Cha 7(2) ina wajibu wa kutoa taarifa sahihi kwa jamii ya watanzania kuhusiana na masuala ya dawa za kulevya na vilevile vyombo vya habari kwa kifungu hiki vinawajibika kutoa habari sahihi kwa wananchi kinyume na hapo ni ukiukwaji wa sheria”amesema Kaji.