***************************
Nteghenjwa Hosseah, Shinyanga
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu OR-TAMISEMI Gerald Mweli ametembelea halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na kukagua eneo la ujenzi wa Ofisi ya Utawala itakayoanzwa kujengwa katika Eneo hilo hivi karibuni.
Halmashauri hiyo ambayo hapo awali Ofisi zake zilikua katika eneo la Utawala la Shinyanga Manispaa wamehamia katika eneo hilo baada ya Agizo la Rais Mhe.Dkt John Pombe Joseph Magufuli lililotolewa Mwezi Oktoba, 2020 la kuzitaka Halmashauri zote zihamie katika maeneo yao ya Utawala.
Akizungumza baada ya kuona eneo la ujenzi lenye ukubwa wa Ekari 20 lililoko katika eneo la Isela Maganzi Mweli amesema amekuja kujiridhisha endapo eneo limeshapatikana, liko sehemu salama na kama kuna madai ya fidia yameshatolewa ili ujenzi wa Ofisi uanze mapema mara tu fedha za ujenzi zitakapotolewa.
‘Hapa nimeridhika eneo ni zuri lina ukubwa wa kutosha na litatosha kwa ujenzi wa Ofisi na maendelea mengine ya Halmashauri hapo baadae’ alisema Mweli
Aidha Mweli alipata nafasi ya kukutana na Menejimenti ya Shinganya Dc na kupata taarifa ya ukusanyaji aa mapato pamoja na utoaji wa mikopo kwa vikundi.
Akiwasilisha taarifa ya mapato Kaimu Mkurugenzi wa Shinyanga Dc amesema makusanyo mpaka kufikia robo ya Pili waliweza kufikia asilimia 30% tu ya lengo walilojiwekea na hii ni kutokana na mapato yao kutegemea zao la pamba ambalo kwa kipindi hicho hali ya haikuwa nzuri.
Pia aliongeza kuwa mikopo iliyotolewa kwa vikundi 8 katika robo ya kwanza ni shilingi Mil. 28 na hivi karibu watatoa shilingi milioni 56 kwa vikundi 5 ambavyo vimepitishwa.
Mweli alitoa angalizo kuwa ukusanyaji wa mapato hauridhishi hata kidogo na kusisitiza kama mapato hayo yanategemea mazao basi waongeze nguvu katika vyanzo vingine ambavyo havitegemei hali ya hewa na kuhakikisha vinakusanywa kwa asilimia 100.
Mweli alimalizia kwa kuwataka Halmashauri ya hiyo kuanza kupima maeneo ya makazi, biashara na Taasisi ili kupanga makao makuu ya Wilaya hiyo na kuendana na kasi ya ukuaji wa mji.