………………………………………………………………………………………
Ikiwa leo ni Siku ya Wanawake Duniani, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda amesema kuazia leo March 08/2020 ataanza kuwashughukikia kikamilifu wanaume wenye tabia ya kuwaonea Wanawake kwa kuwapiga hadi kuwaharibu mwonekano wa sura,macho,kuwavunja meno au taya na kusababisha baadhi yao kupata ulemavu wa kudumu jambo ambalo ni kinyume na Sheria.
RC Makonda amesema Mwanamke yoyote atakaeshushiwa kipigo na Mwanaume kuanzia sasa atoe taarifa kupitia simu ya mkononi namba 0682009009 ili mwanaume alietenda ukatili huo atafutwe popote alipo na kuchukuliwa hatua Kali za kisheria.
Aidha RC Makonda amesema baadhi ya Wanaume wamekuwa na tabia ya kuwadharau wanawake kutokana kutokuwa na elimu au kipato jambo ambalo amesema hawezi kulivumilia katika mkoa huo.
Katika hatua nyingine RC Makonda amesema amepanga kuliomba Bunge linapofanya Mabadiliko ya Sheria ya ndoa kiongezwe kipengele cha kutaka 40% ya Mshahara wa Mwanaume apatiwe mwanamke asiefanya kazi kwaajili ya Shughuli za familia ili kumjengea uwezo Mwanamke.
Pamoja na hayo RC Makonda amewataka Wanawake kutojisahau katika suala zima la malezi ili kuwaepusha watoto na makundi mabaya ikiwemo Matumizi ya Dawa za kulevya, Ushoga, Usagaji, Wizi na Uporaji.