Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusiana na kukamatwa kwa wahalifu , dawa za kulevya na zana haramu za uvuvi.Picha na Baltazar Mashaka
NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza
KIGOGO na kinara wa uingizaji na usambazaji wa zana haramu za uvuvi katika Ziwa Victoria , Jeremiah Asama ( 48),mkazi wa Bwiru, Manispaa ya Ilemela ni miongoni mwa watu sita wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Mwanza, huku mtuhumiwa wa saba akidaiwa kutoroka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro alisema juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukamatwa kwa watu hao wakiwemo askari wanne wa jeshi hilo wanaodaiwa kukiuka maadili ya kazi yao.
Alisema wanawashikilia watu sita kwa makosa ya kupatikana na zana haramu za uvuvi, dawa za kulevya (bhangi na mirungi) ambapo pia linachunguza askari wanne kuona kama kulikuwa na ukiukwaji wa maadili ya kazi wakati wa kuwakamata watuhumiwa hao.
Muliro alisema kuwa jeshi hilo limejikita kuwakamata wahalifu wa makosa makubwa (wasambazaji) ili kuondokana na mfumo wa kukimbizana na wavuvi na wahalifu wadogo wadogo ambapo taarifa wanazopata kutoka kwa wananchi zinalenga kuzuia vitendo vya uhalifu mkoani humu.
Alisema kuwa machi 5, mwaka huu, askari walimkamata Omolo pamoja na wake zake wawili Joyce Jermiah (40) na Getrude David (26), wakiwa na mali haramu kinyume cha sheria za uvuvi na alipopekuliwa nyumbani kwake eneo la bwiru alikutwa akiwa na nyavu aina ya Gillnet 7,401, Monofilament timber 178, makokoro matatu za dagaa na Roler moja ya kokoro hizo zikiwa zimefichwa darini.
Kamanda huyo wa polisi alisema kuwa mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwa kinara wa uingizaji na usambazaji wa zana hizo haramu za uvuvi kwenye maeneo mbalimbali ya ziwa victoria na laiti nyavu hizo zingeingia ziwani ni wazi zingesababisha madhara makubwa kwa rasilimali za uvuvi hasa mazao ya samaki.
Hata hivyo baada ya watuhumiwa hao kukamatwa, yalijitokea madai yaliyowalenga baadhi ya askari polisi wakidaiwa kukiuka maadili ya utendaji wa kazi ambapo uchunguzi juu ya madai hayo unafanywa kwa kufuata mfumo wa kijeshi na ikibainika hatua za kinidhamu za kijeshi zitachukuliwa.
Inadaiwa na chanzo chetu kuwa kabla ya tukio la kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo askari polisi wanne (majina yanahifadhiwa), walikwenda dukani kwake Mta wa Libert wilayania Nyamagana kwa nia ya kumkamata baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa anaingiza na kusambaza zana haramu za uvuvi.
Askari hao baada ya kwenda dukani kwa mtuhumiwa waliingia kwenye majadiliano wakamshawishi awape hongo ya sh. milioni 20 ili wamwachie na katika majadiliano hayo walikubaliana awape sh. milioni 8 ambapo wanadaiwa kupokea sh. milioni 4.
Baada ya kupewa kiasi hicho walichukua kielelezo cha zana hizo haramu hadi kituo na kumtaka aongeze kiasi ch fedha kilichosalia vinginevyo wangemfikisha mahakamani ndipo ulipoandaliwa mtego wa kuwanasa.
Kauli ya Muliro
Akitoa ufafanuzi wa kadhia hiyo ya rushwa Muliro alisema; “Siwezi kusema hilo mnalosema ninyi, naweza kukulisha kwa mkono wa kulia kisha nikakunyang’anya kwa mkono wa kushoto.Unaweza kufanya vizuri sana lakini uka- overloock, ukafanya bila kuwa na Such Older, ni ukukwaji wa maadili na hivyo tutaangalia na bado tunachunguza.”
Alieleza kuwa jeshi hilo linawashikilia na kuwahoji askari wanne wanaodaiwa kukiuka maadili ya utendaji wakati wakiwakamata watuhumiwa (Asama na wake zake wawili) na kwamba wanawachunguza kupitia mfumo wa utendaji unaohusu ukiukwaji wa maadili ili kuona, kwani huenda wakati wakitekeleza majukumu yao wali overloock.
Kwa mujibu wa Muliro mfumo wa jeshi uko wazi wa kuwahoji askari hao na ikithibitika hatua za kinidhamu zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwafikisha kwenye Mahakama ya Kijeshi (Court Marshall) ambapo kwa sasa sual hilo liko kwenye Baraza la Kijeshi ambalo linajua jinsi ya kuchunguza madai na tuhuma za aina hiyo.SSSSS
Kinara wa usambazaji, uingizaji Mirungi anaswa
NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA
Jeshi la Polisi jijini Mwanza, limefanikiwa kumtia mbaroni kinara wa usafirishaji na muuzaji maarufu wa madawa ya kulevya aina ya mirungi,Peter Charles Mwita @ Peter Mirungi(46)mkazi wa Mtaa wa Rufiji, kwa makosa ya kusafirisha, kusambaza na kuuza mirungi jijini Mwanza.
Mbali na Peter jeshi hilo linawashilia watu wengine wawili kwa tuhuma za namna hiyo huku mmoja akiwakimbia polisi baada ya kuruka kutoka ndani ya gari alilokuwa akiliendesha kwenye kizuizi cha Ngashe Kata ya Lugeye, wilayani Magu.
Mtuhumiwa huyo ambaye amelisumbua jeshi hilo ka miaka mingi baada ya kubaini anafuatiliwa na polisi, Februari 1, mwaka huu alitelekeza gari lake namba T.787 DQX aina ya Probox eneo la Igoma Mashariki, likiwa na mirungi kg 9.02.
Pia Februari 15, Peter ambaye amekuwa akifanya biashara hiyo haramu kwa muda mrefu baada ya kuwakimbia polisi aliangukia na mkono wa dola.
Aidha Machi 2, mwaka huu majira ya 12:00 asubuhi huko kwenye kizuizi cha magari kilichopo Katika Kijiji cha Ngashe, Kata ya Lugeye, wilayani Magu, askari wa doria walikamata bhangi kg 50, zikiwa kwenye magunia matatu, ndani ya gari lenye namba za usajili T.881 AFX na tela namba T.822 CZZ Lori aina ya scania.
Gari hilo lilikuwa likitokea Tarime kuja jijini Mwanza, likiendeshwa na dereva aliyetambulika kwa jina la Joseph Achiyo ambaye aliruka kwenye gari na kukimbia baada ya kusimamishwa na askari. 28
Pia Faustine Koroso (46) mkazi wa Nyakato Mashariki na Gidion Paul (28) mkazi wa Igoma walikamatwa na polisi eneo la Nyakato Sokoni Machi 2, mwaka huu majira ya 12:30 jioni wakisafirisha mirungi kg 20 kwa kutumia pikipiki aina ya HONLG yenye namba za usajili MC 931CKL.
Kwa mujibu wa Muliro polisi wanaendelea na mahojiano dhidi ya watuhumiwa wote baada ya kukamilika kwa uchunguzi watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo na kuwaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo sheria.
Pia amewaonya waendesha pikipiki za bodaboda wanaojihusisha na usafirishaji wa madawa ya kulevya kuwa wanachafua taswira ya biashara yao na wasithubutu kujiingiza kwenye mfumo huo.