Mwenyekiti wa Kamati ya bunge ya kudumu ya masuala ya Ukimwi,Kifua Kikuu na Dawa za kulevya Mhe.Oscar Mukasa,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma kuelekea kwenye uzinduzi wa kampeni endelevu ya kupinga unyanyapaa na Mapambano dhidi Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi itakayofanyika siku ya Jumatatu Machi 9 na mgeni rasmi anatarajia kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa,kulia kwake ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi(NACOPHA),Bw.Deogratius Rutatwa
Mwenyekiti wa Kamati ya bunge ya kudumu ya masuala ya Ukimwi,Kifua Kikuu na Dawa za kulevya Mhe.Oscar Mukasa,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma kulia kwake ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi(NACOPHA),Bw.Deogratius Rutatwa
Sehemu ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakifatilia hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ya bunge ya kudumu ya masuala ya Ukimwi,Kifua Kikuu na Dawa za kulevya Mhe.Oscar Mukasa,alipokuwa akitoa taarifa kuelekea kwenye uzinduzi wa kampeni endelevu ya kupinga unyanyapaa na Mapambano dhidi Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi itakayofanyika siku ya Jumatatu Machi 9 jijini Dodoma.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi(NACOPHA),Bw.Deogratius Rutatwa,akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuelekea kwenye uzinduzi wa kampeni endelevu ya kupinga unyanyapaa na Mapambano dhidi Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi itakayofanyika siku ya Jumatatu Machi 9 jijini Dodoma.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi(NACOPHA) ,Bw.Deogratius Rutatwa,akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuelekea kwenye uzinduzi wa kampeni endelevu ya kupinga unyanyapaa na Mapambano dhidi Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi itakayofanyika siku ya Jumatatu Machi 9 jijini Dodoma.
…………………………………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua kampeni endelevu ya kupinga unyanyapaa kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi na Kifua Kikuu(TB) Machi 9, mwaka huu jijini Dodoma.
Kampeni hiyo inafanywa na Serikali kwa kushirikiana na Bunge na Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi(NACOPHA) ambapo uzinduzi huo utawakutanisha viongozi wa dini nchini ili kusaidia kupinga unyanyapaa.
Akizungumza leo na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya masuala ya Ukimwi, TB na dawa za kulevya, Oscar Mukasa, amesema Spika wa Bunge, Job Ndugai atakuwa mwenyeji wa tukio hilo ambalo litafanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa Bungeni jijini Dodoma.
Mwenyekiti huyo amesema wameamua kutumia viongozi hao kutokana na asilimia 90 ya watanzania wanaabudu kwenye madhehebu mbalimbali ya dini hivyo itakuwa rahisi kutoa elimu kwa jamii.
Amesema unyanyapaa ni miongoni mwa vikwazo vinavyosababisha kutofikia malengo ya kidunia kutokana na watu wengi kuogopa kupima na kupata majibu ili kuanza tiba.
“Spika atakuwa mwenyeji katika kikao kitakachowakutanisha viongozi wa dini kwa ajili ya kushirikiana na Bunge kwenye mapambano ya Ukimwi hususan unyanyapaa kwa kuwa malengo ya kidunia yanataka ifikapo mwaka 2025 tuwe tumefikia 95-95-95,”amesema.
Amesema asilimia 95 ya kwanza inataka watanzania wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi(VVU) wawe wanatambua afya zao.
“Asilimia 95 ya pili inataka wawe wameingia kwenye mpango wa kupatiwa tiba na matunzo, na asilimia 95 wanatakiwa kutumia vizuri tiba wanayopata kufubaza vidudu,”amebainisha.
Hata hivyo, amesema kwasasa Tanzania katika 95 ya kwanza ipo asilimia 62 huku 95 ya pili na tatu ipo zaidi ya asilimia 90.
“Unyanyapaa unasababisha kutofikia asilimia 95 ya kwanza ya kujua hali zetu, sasa kwanini tumeamua kutumia viongozi wa dini kwa kuwa wana majukwaa yanayounganisha watanzania wengi sana,”amesisitiza.
Naye, Afisa Mtendaji Mkuu Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi(NACOPHA), Deogratius Rutatwa, amesema kampeni hiyo inalenga kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya kidunia na kuwa na kutokuwa na unyanyapaa.
“Hatutaweza kufikia 95 tatu kama hatutaondoa unyanyapaa kwasababu hata waliopo kwenye tiba wanakimbia kutokana na unyanyapaa, na mwingine anaficha dawa au kuogopa kunyonyesha akiogopa kunyooshewa vidole,”amesema.
Amesema viongozi hao wana nafasi kubwa ya kuchangia na kuweka mabadiliko katika mapambano ya unyanyapaa.
“Tutakuwa na kiongozi wa dini kutoka Uganda ambaye anaishi na VVU, Mbunge pia anayetoka Zambia anayeishi na VVU ili wazungumze uzoefu wao katika kuishi na VVU tutaka watu wafunguke na hapa Tanzania kwa kuwa Ukimwi hauchagui,”amesema.
Aidha, ameshukuru serikali ya Marekani kupitia Mfuko wa Rais wa kupambana na Ukimwi ( PEPFAR) na Shirika lake la USAID kwa kufadhili kampeni hiyo kupitia mpango mahsusi wa kuhakikisha viongozi wa dini wanashiriki kwenye mapambano ya kupinga unyanyapaa na kuhakikisha usalama kwa watoto.