Home Mchanganyiko THBUB YAMPONGEZA RAIS DKT.MAGUFULI KUKUTANA NA VIONGOZI WA VYAMA VYA UPINZANI

THBUB YAMPONGEZA RAIS DKT.MAGUFULI KUKUTANA NA VIONGOZI WA VYAMA VYA UPINZANI

0

……………………………………………………………………………….

Itakumbukwa kuwa mapema wiki hii Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi watatu wa vyama vya upinzani. 

Viongozi hao ni Mshauri wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalimu Seif Sharif Hamad, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Bwana James Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). 

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inapenda kuchukua fursa hii kumpongeza kwa dhati Mhe. Rais kwa hatua yake hiyo ya kizalendo na muhimu kwa ustawi wa nchi yetu.

Hatua hiyo ya Mhe. Rais ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya upinzani ni kielelezo cha kukua kwa utawala bora nchini.

Aidha, Tume imefurahishwa na ahadi aliyoitoa Mhe. Rais katika mazungumzo hayo ikiwa ni kwa mara ya pili baada ya kutoa kauli kama hiyo kwa Mabalozi wawakilishi wa nchi zao, katika ghafla ya kuanza mwaka mpya, kuwa uchaguzi mkuu ujao utakuwa huru na wa haki. Bila shaka kauli hiyo inaonyesha dhamira aliyonayo Mhe. Rais na Serikali yake katika kuhakikisha kuwa demokrasia, amani na utulivu vinaendelea kushamiri hapa nchini – tunampongeza sana!

Kwa kauli hiyo ya Mhe. Rais, Tume inaamini kuwa taasisi zenye dhamana ya kusimamia uchaguzi mkuu ujao na wadau wa uchaguzi watachukua hatua mahsusi za kuhakikisha kuwa azma ya Mhe. Rais inatimia.

Ni matumaini ya Tume kuwa hatua ya Mhe. Rais ya kufungua milango kwa viongozi wa vyama vya upinzani itakuwa endelevu.

Tume inamwomba Mhe. Rais kuendeleza utaratibu huo wa kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani na makundi mengine pindi nafasi ya kufanya hivyo itakaporuhusu.