Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Maswa Venance Salia akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Bariadi wakati walipokuwa wakiupokea msafara wa kijinsia ulipofika Wilayani humo.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Bi. Imelda Kamugisha akieleza Lengo la Msafara wa kijinsia wakati ulipopokelewa katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu.
Msafara wa Kijinsia wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu mara baada ya kuupokea Msafara wa kijinsia ulipofika Wilayani humo.
Wasanii Shetta, G Nako na Motrathefuture wakitumbuiza katika Stendi ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wakati Msafara wa kijinsia ulipofika wilayani hapo.
Kikundi cha ngoma cha Wilayani Maswa kikitumbuiza wakati wa mapokezi ya Msafara katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
***************************
Na Mwandishi Wetu Maswa
Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Maswa Venance Salia amesema kuwa Serikali ya Wilaya haitawavumilia watendaji wa vitendo vya ukatili kwani hawatakuwa salama katika Wilaya hiyo.
Ameyasema hayo wakati akiupokea msafara wa kijinsia Wilayani Maswa wenye lengo la kutoa elimu ya madhara ya vitendo vya kikatili nchini.
Ameongeza kuwa kwa kipindi cha mwaka 2018 jumla ya matukio 466 yaliripotiwa na kwa mwaka 2019 kumekuwa na matukio takribani 674 ya vitendo vya ukatili vikiwemo vipigo, unyanyasaji na mimba na ndoa za utotoni.
“Sisi tunasema hawatakuwa salama hawako salama wale wote wanaofanya vitendo vya kikatili iwe kwa wanawake watoto hata wanaume tutawashughulikia” alisema
Bw. Salia amesema kuwa Wilaya ya Maswa imezidhatiti katika kupambana na vitendo vya kikatili na kwa kuanzia Januari hadi Desemba mwaka 2019 jumla ya kesi 42 zimeripotiwa na watuhumiwa 15 wamehukumiwa kwa kifungo cha miaka 30 jela.
“Tumewaweka ndani waharibifu hao hapa ukibainika tu umefanya kitendo cha kikatili basi Sheria itachukua mkondo wake” alisema
Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Bi Imelda Kamugisha amesema kuwa lengo kuu la msafara wa kijinsia ni kutoa elimu juu ya madhara ya vitendo vya ukatili nchini.
Ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kutokomeza vitendo vya kikatili katika jamii hivyo ameitaka jamii kushiriki katika kupambana kwa nguvu ili kuondokana na vitendo hivyo.