Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akiongea wakati akifungua mafunzo ya jinsi ya kuepuka maambukizi ya Virusi vya Corona kwa viongozi wa dini mbalimbali waliojitokeza katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar Es Salaam.
Mwakilishi mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Tigest Katisela akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa viongozi wa dini kuhusiana na jinsi ya kuepuka maambukizi ya ugonjwa wa Corona usiingie nchini.
Mwakilishi mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Tigest Katisela akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa viongozi wa dini kuhusiana na jinsi ya kuepuka maambukizi ya ugonjwa wa Corona usiingie nchini.
Baadhi ya viongozi wa dini waliofika katika mafunzo ya jinsi ya kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Corona unaoendelea kusambaa duniani. Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Afya na kushirikisha viongozi wa dini mbalimbali nchini.
Picha ya pamoja ya Waziri Ummy Mwalimu akiwa na viongozi wa dini na wadau mbalimbali wa maendeleo waliofika katika mafunzo ya namna ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona yanayofanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar Es Salaam.
………………………………….
Waziri Ummy Mwalimu ametoa masaa 5 kwa kila Halmashauri kutenga sehemu maalum kwaajili ya kumuweka mshukiwa wa ugonjwa wa Corona na kufanya utaratibu wa uchunguzi na kutoa taarifa haraka Wizara ya Afya.
Waziri Ummy ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo kwa viongozi wa dini nchini jinsi ya kuepuka maambukizi ya Virusi vya Corona ambavyo vinazidi kusambaa katika nchi mbalimbali duniani. “Ninatoa muda mpaka saa 10 jioni vituo vyote vya afya vya umma nchini viwe vimetenga sehemu maalum ya kuweka mshukiwa wa Virusi vya Corona na kuripoti haraka iwezekanavyo katika Wizara ya Afya kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki”. Amesema Mhe. Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy amesema mpaka sasa nchi yetu ni salama, hakuna mshukiwa wa COVID19 lakini Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kudhibiti ugonjwa huu usiingie nchini ikiwa ni pamoja na kushirikisha taasisi mbalimbali za dini. “Tunawaomba viongozi wa dini muende mkatoe elimu kwa waumini wenu kuchukua tahadhari kwa kuzingatia kanuni za usafi na pia kukaa mbali na mtu mwenye dalili za mafua ambaye ana historia ya kusafiri nje ya nchi”. Mhe. Ummy.
Aidha, Waziri Ummy ametoa maelekezo kwa taasisi za dini, taasisi za umma, maofisi na mashule ya Serikali na binafsi kuweka sehemu maalum ya kunawa mikono kwa maji yenye dawa ya kuua bakteria (hand sanitizers) ili kuepuka maambukizi yatokanayo na bakteria.