Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Leonard Subi akisema jambo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya na viongozi waandamizi wa Jeshi la Magereza nchini (hawapo pichani).
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya pamoja na wataala kwenye kikao cha pamoja wakijadiliana masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya gerezani katika kikao kilichoongzowa na Mwenyekiti Mhe. Oscar Mukasa.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya wakisalimiana na maafisa wa Gereza kuu la Arusha walipofanya ziara gerezani hapo kuzungumza na wafungwa na mahabusu.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee akisema jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya (hawapo pichani) wakati wa ziara katika Gereza Kuu la Arusha.
…………………………………………………………………………………………
Na Englibert Kayombo WAMJW – Arusha
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi amesema kuwa Tanzania haina upungufu wa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV)
Dkt. Subi amesema kauli hiyo leo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi na Madawa ya Kulevya walipofanya ziara ya pamoja kutembelea Gereza la Arusha (Kisongo)
“Hatuna upungufu wa dawa za ARV Tanzania na hatujawahi kuwa na upungufu wa dawa hizo zaidi miaka kumi iliyopita” amesema Dkt. Subi
Amesema kuwa upatikanaji wa dawa za ARV umekuwa ni wa uhakika na wagonjwa wote wanapata dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi.
“Ni kweli kuna baadhi ya dawa hasa za magonjwa nyemelezi, kuna muda kulikuwa na upungufu lakini hivi sasa tuna dawa za kutosha” amesema Dkt. Subi
Dkt. Subi ametolea mfano katika Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD), dawa ya “Ceptrin” kwa nchi nzima viko vidonge zaidi ya Milioni 62, ambapo kwa kanda ya Kaskazini wakiwa na vidonge Milioni 8.6 huku dawa za watoto zikiwa ni 786,000.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Magereza nchini Suleiman Mzee amesema kuwa Jeshi la magereza ni moja ya wahanga wa ugonjwa wa VVU/Ukimwi, na hawapo nyuma katika kupambana na ugonjwa huo kwa wafungwa, mahabusu, watumishi na familia zao.
Kamishna Mzee amesema kuwa Jeshi la magereza linatoa huduma za uchunguzi wa afya, tiba, ushauri nasaha na upimaji wa virusi vya ukimwi pamoja na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
“Jeshi la Magereza lina jukumu la kuhakikisha wafungwa na mahabusu wanapata huduma bora za afya kama ilivyo kwenye jamii nyingine” amesema Kamishna Suleiman Mzee.