Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na Waandishi wa habari(hawapo pichani) Ofisini kwake Mjini Bariadi, kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Kitaifa yanayofanyika Mkoani Simiyu pamoja Ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
……………………………………………………………………………………………
Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo Kitaifa yatafanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake Mjini Bariadi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli Mbiu “Kizazi cha Usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya Sasa na ya baadaye” ambapo yataanza tarehe 02 Machi 2020 mpaka tarehe 08 Machi 2020.
“Katika Maadhimisho haya tunawatarajia wageni mbalimbali na shughuli mbalimbali kufanyika; mathalani kuanzia Tarehe 02 Machi 2020 maonesho ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wanawake zitaoneshwa, wajasiriamali kutoka maeneo yote nchini wamethibitisha kushiriki pia kutakuwa na upimaji kwa magonjwa mbalimbali ya Wanawake,”
“Siku ya tarehe 06 Machi 2020 kutakuwa na Jioni ya mwanamke ambapo wake za Viongozi waliopo madarakani na wastaafu na Watendaji mbalimbali wa Taasisi watashiriki; mpaka sasa Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu wa Awamu ya nne, Mama Tunu Pinda, Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Tanzania na viongozi mbalimbali Wanawake wamethibitisha kushiriki, wakiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe.Ummy Mwalimu,” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu kushiriki katika shughuli zote zitakazofanyika katika Wiki ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Kitaifa na kilele chake ambazo zitafanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Katika hatua nyingine Mtaka amesema Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya siku tatu Mkoani Simiyu kuanzia tarehe 06 Machi 2020 hadi 08 Machi 2020.
Amesema tarehe 06 Machi, 2020 Mhe. Makamu wa Rais atafungua Tawi la Benki ya NMB katika Kata ya Nyashimo makao Makuu ya Wilaya ya Busega na baadaye kuweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Tawi la Chuo cha Usimamizi (IFM), katika Kata ya Sapiwi wilayani Bariadi.
Ameongeza kuwa tarehe 07 Machi, 2020 Mhe. Makamu wa Rais atafungua Ofisi ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ya Mkoa na siku hiyo hiyo ataweka jiwe la msingi Ujenzi wa Kituo cha Mabasi cha Halmashauri ya Mji wa Bariadi kilichopo Kata ya Somanda.
“Nitumie nafasi kuwaomba Wananchi wa Mkoa wa Simiyu hususani katika maeneo yote ambayo Mhe. Makamu wa Rais atapita kujitokeza kwa wingi kumsikiliza kwa kuwa katika maeneo yote ambayo Mhe. Makamu wa Rais atafungua na kuweka mawe ya msingi miradi, atazungumza na wananchi, ” alisema Mtaka.
Mhe. Makamu wa Rais atahitimisha ziara yake Mkoani Simiyu tarehe 08 Machi kwa kuwaongoza wananchi katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Kitaifa.