TANZANIA imetanguliza mguu mmoja mbele katika mbio za kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia kwa Wanawake chini ya umri wa miaka 17 baadaye mwaka huu India baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Uganda jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Sasa Tanzania itahitaji kwenda kuulinda ushindi wake mwembamba kwenye mchezo wa marudiano Machi 13 Jijini Kampala ili isonge mbele ambako itakutana na mshindi kati ya Sao Tome Príncipe na Cameroon.
Haukuwa ushindi mwepesi kwa Tanzania leo baada ya kutanguliwa na Uganda kwa bao la dakika ya tano tu la Faudhia Najjemba aliyepiga shuti kali akimalizia pasi ndefu ya Margret Kunihira.
Tanzania ikasawazisha bao hilo dakika ya 28 kupitia kwa mshambuliaji wake Aisha Masaka aliyepiga shuti kali pia kumalizia kazi nzuri ya Irene Kisisa.
Dakika ya 85 Aisha Masaka akapiga nje mkwaju wa penalti ulitolewa na refa Ema Paulo Novo kutoka Msumbiji baada ya yeye mwenyewe kuchezewa rafu na Bira Nadunga wa Uganda.
Hata hivyo, binti huyo ambaye tayari ameanza kukomazwa kwenye kikosi cha wakubwa, Twiga Stars akasawazisha makosa yake kwa kufunga bao la ushindi dakika mbili baadaye akimalizia pasi ya Christer Bahera.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Asha Rashid, Neema Shibara, Protasia Mgunda, Fumukazi Ally, Ester Mabanza, Lucia Mrema, Aisha Khamis, Emeliana Isaya, Christer John, Irene Kisisa na Rose Mpoma/Joyce Charles dk72.
Uganda: Daphine Nyayenga, Sumaya Komuntale, Margret Kunihira, Catherine Nagadya, Shakira Nyinagahirwa, Samalie Nakacwa, Nalikenge juliet, Aluka Grace/Namugerwa Gloria dk81, Hadija Nandago/Zainab Nandede dk72, Fauzia Najjemba na Bira Naduga.