Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akiongea katika kikao cha majadiliano kilichowakutanisha ujumbe wa THBUB na Viongozi wa LHRC kwenye ofisi za kituo hicho jijini Dodoma leo (Februari 27, 2020). Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga.
Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi wa Ujenzi wa Uwezo na Ufuatiliaji kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Felista Mauya muda mfupi baada kumaliza kikao cha majadiliano kilichowakutanisha ujumbe wa THBUB na Viongozi wa LHRC kwenye ofisi za kituo hicho jijini Dodoma leo (Februari 27, 2020).
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga (katikati) akijibu baadhi ya hoja zilizoibuka katika kikao cha majadiliano kilichowakutanisha ujumbe wa THBUB na Viongozi wa LHRC kwenye ofisi za kituo hicho jijini Dodoma leo (Februari 27, 2020). Kulia ni Mwenyekiti wa
THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu. Kushoto ni Mkurugenzi wa Ujenzi wa Uwezo na Ufuatiliaji kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Felista Mauya.
****************************
Na Mbaraka Kambona,
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wamekubaliana kuandaa mpango wa pamoja wa kutoa elimu katika mashuleni ili kuhamasisha na kukuza haki za binadamu nchini.
Makubaliano hayo yalifikiwa na pande zote mbili baada ya majadiliano yaliyofanyika katika kikao kilichowakutanisha ujumbe wa THBUB na Viongozi wa LHRC kwenye ofisi za kituo hicho jijini Dodoma leo.
Akiongea katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma, Mafunzo, Utafiti na Nyaraka wa THBUB, Alexander Hassan alisema kuwa ili ushirikiano wa THBUB na LHRC
uwe na tija ni vyema kuunganisha nguvu katika maeneo wanayofanya kazi zinazofanana.
Alexander alisema kwakuwa taasisi zote mbili zimeanzisha Klabu za haki za binadamu mashuleni ni vyema kuunganisha nguvu katika maeneo hayo ili kupata matokeo makubwa zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga akichangia hoja hiyo alisema kuwa suala hilo la kuunganisha nguvu ni zuri na ni muhimu likafanyiwa kazi kwa haraka na kama uongozi wa THBUB utaridhia basi maafisa wa pande zote mbili wakutane mapema iwezekanavyo ili kuandaa mpango huo.
Henga alisema kuwa LHRC kwa muda mrefu imekuwa ikitoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya haki za binadamu kwa njia mbalimbali ikiwemo matumizi ya vyombo vya habari, vipeperushi na mikutano ya hadhara na hivyo kuwafikia watu wengi lakini ni muhimu kwa
sasa kuunganisha nguvu na THBUB ili kuepuka kutawanya nguvu na rasilimali kwa mambo ambayo wanaweza kufanya kwa pamoja.
Henga alisema kuwa wamefurahishwa na kuteuliwa kwa Makamishna wa THBUB kwani kutasaidia wananchi kupata haki zao na ushirikiano wa wadau utaimarika zaidi.
Alisema kwa kuanza mpango huo itakuwa vyema kama watashirikiana kwa pamoja kuimarisha elimu ya haki za binadamu katika klabu za mashuleni kwani wakifanikiwa
kuelimisha watoto shuleni wataweza kusimama na kutetea haki zao wenyewe.
Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu alisema katika kikao hicho kuwa THBUB inatambua mchango mkubwa wa LHRC katika kukuza na kutetea haki za binadamu na alimuhakikishia Mkurugenzi wa kituo hicho kuwa tume itaendelea kushirikiana kwa karibu na kituo hicho kwa kuwa wote lengo lao ni kusaidia wananchi kupata haki zao.
Aidha, alisisitiza kuwa katika kutekeleza majukumu yao ni vyema kujikita kusaidia jamii na serikali kwa ujumla kutekeleza majukumu yake, pale ambapo serikali inafanya vizuri ni vyema kupongeza na pale inapoonekana imekosea basi ni vyema kutafuta namna nzuri ya kukosoa.