Home Mchanganyiko SHULE YA MSINGI RAMADHANI YANUFAIKA NA UJENZI WA BARABARA YA NJOMBE-MORONGA (KM...

SHULE YA MSINGI RAMADHANI YANUFAIKA NA UJENZI WA BARABARA YA NJOMBE-MORONGA (KM 53.9)

0

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, uchukuzi na Mawasiliano, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, akisalimiana na wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Ramadhan mkoani Njombe, alipofika kukagua ujenzi wa
madarasa na bwalo liliojengwa na mkandarasi CHICO anayejenga mradi wa ujenzi wa barabara ya Njombe- Makete sehemu ya Njombe -Moronga (Km 53.9).

Mhandisi Mshauri, akionesha bwalo lilojengwa na mkandarasi CHICO anayejenga barabara ya Njombe- Makete sehemu ya Njombe -Moronga (km 53.9). Ujenzi wa jengo hilo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo ambapo inahusisha ujenzi wa bwalo moja na vyumba vya madarasa viwili kwa gharama ya shilingi milioni 280.

Vyumba vya madarasa vikiwa vimekamilika ambavyo vimejengwa na mkandarasi CHICO anayejenga barabara ya Njombe- Makete sehemu ya Njombe -Moronga (Km 53.9). Ujenzi wa jengo hilo ni ahadi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la
ujenzi wa barabara hiyo.

Muonekano wa ndani wa bwalo jipya la chakula ambalo limejengwa na mkandarasi CHICO anayejenga barabara ya Njombe- Makete sehemu ya Njombe -Moronga (Km 53.9). Ujenzi wa jengo hilo ni ahadi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la
ujenzi wa barabara hiyo.

Muonekano wa barabara ya Njombe- Makete sehemu ya Njombe – Moronga (km 53.9). Barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi CHICO ambapo kwa sasa imefika asilimia 64.

PICHA NA WUUM

***************************

Shule ya Msingi ya Ramadhani iliyopo mkoani Njombe imenufaika na mradi wa ujenzi wa barabara ya Njombe- Makete sehemu ya Njombe -Moronga (km 53.9) kwa kujengewa madarasa mawili na bwalo litakalotumika kwa
matumizi mbalimbali.

 

Ujenzi wa majengo hayo ni ahadi ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika barabara hiyo kwa kuahidi kutatua changamoto zilizokuwa zinakabili shule hiyo ikiwemo kukosekana kwa bwalo la kulia chakula katika kipindi cha mvua pamoja na upungufu wa vyumba vya madarasa.

 

Akikagua mradi huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, amefurahishwa na kiwango cha ujenzi wa majengo hayo ambayo yamekamilika kwa kiwango
bora ambapo pia yamezingatia ujenzi wa njia za wanafunzi wenye uhitaji maalumu.

 

Aidha, Mwakalinga amewapongeza wakazi wa eneo hilo kwa kujitoa kuongeza vyumba vya madarasa viwili na ofisi moja ya walimu kwa nguvu zao wenyewe na amewaasa wananchi wa sehemu nyingine kuiga mfano kama huo ili kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais.

 

“Nawapongeza sana wazazi wenye watoto wao hapa kwa kujitoa kuongeza vyumba vya madarasa, pia naomba Mkandarasi Mshauri usimamie majengo haya na kutoa ushauri wa kitaalamu ili yaendane na viwango vya
majengo mliyoyajenga nyinyi”, amesema Mwakalinga.

 

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ephraim Sanga, ameishukuru serikali kwa kufanikisha ujenzi huo kwa wakati kwani shule hiyo ina idadi kubwa ya wanafunzi ukilinganisha na idadi ya madarasa na hivyo kupelekea
wanafunzi kurundikana katika vyumba vya madarasa na kukosekana kwa ufaulu mzuri wa masomo yao.

 

Ameongeza kuwa kauli ya Rais Magufuli imekuwa tiba kwao, kwani tayari mradi huo umeshakamilika na kwa sasa wanachokisubiri ni kukabidhiwa kwa majengo hayo kutoka kwa mamlaka husika.

 

Katika hatua nyingine Mwakalinga amekagua Barabara ya Njombe- Makete sehemu ya Njombe- Moronga (Km53.9) inayojengwa na mkadari M/s China Henan International Group company na Barabara ya Itoni-Ludewa -Manda
sehemu ya Lusitu – Mawengi (Km 50) ambayo inajengwa na mkandarasi M/S Cheon Kwang Engineering & construction Co. Ltd.

 

Mwakalinga, amewataka makandarasi hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa mkataba ikiwemo kukamilisha barabara hizo kwa  wakati na kwa viwango vinavyokubalika na kwamba uwepo wa vipindi vya mvua isiwe ni kisingizio cha wao kutofanya kazi.

 

“Ujenzi wa Barabara unahusisha kazi nyingi, kuna baadhi ya kazi hata kukiwa na mvua zinaendelea kufanyika, msiache kufanya kazi kwa kisingizio cha mvua, Jambo hili sitaki kulisikia”, amesisitiza Mwakalinga.

 

Katibu Mkuu Mwakalinga, yupo katika ziara ya kizazi ya siku Tatu mkoani Njombe, ambapo pamoja na mambo mengine amekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Sekta yake pamoja na kuangalia athari za mvua katika
miundombinu ya barabara.