Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni akizungumza katika Mkutano wa Mashauriano ulioandaliwa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu- Uwekezaji,ukiwajumuisha wafanyabiashara na wawekezaji katika mkoa wa Simiyu.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Na Mwandishi Wetu, Simiyu
Serikali imesema imefanikiwa kudhibiti matukio ya uporwaji fedha kwa wafanyabiashara na wawekezaji huku ikiwa na mkakati maalumu wa kuhakikisha wawekezaji na wafanyabiashara wanafanya shughuli zao za maendeleo kwa amani na utulivu pasina shaka yoyote.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni wakati akizungumza katika mkutano wa mashauriano ulioandaliwa na Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji,Angellah Kairuki ukiwaalika wafanyabiashara na wawekezaji katika mkoa wa Simiyu.
“Kuanzia Januari mwaka jana mpaka sasa tulipo matukio ya unyang’anyi kwa kutumia silaha yameripotiwa kuwa ni tukio moja moja katika Mkoa wa Songwe,Tabora,Njombe,Mjini Magharibi,Temeke na Kinondoni na tayari watuhumiwa ishirini na mbili washamakamatwa na kesi zao ziko mahakamani zikiendelea na utaratibu wa kisheria” alisema Masauni
Masauni aliweka wazi sababu ya mafanikio hayo ni mafunzo mbalimbali waliyopewa askari wa Jeshi la Polisi ambayo yanawawezesha kupambana na aina tofauti za uhalifu hali inayopelekea kupungua na kuisha kwa matukio hayo.
“Kipindi cha nyuma mmeshuhudia wafanyabiashara na wawekezaji wakivamiwa na majambazi na kuporwa kiasi kikubwa cha fedha aidha wakiwa wanaenda kuzihifadhi benki au kwa kuvamiwa nyumbani,Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama kwa kupitia intelijinsia wamekua wakifanikiwa kiudhibiti matukio hayo na sasa tumeona katika Awamu hii ya Serikali ya Tano matukio hayo yamepotea kabisa na niwaombe wawekezaji pamoja na wafanyabiashara nchi nzima waendelee na shughuli zao pasina kuwa na shaka yoyote” alisema Masauni
Akitaja idadi ya matukio ya unyang’anyi wa fedha kuanzia Januari mwaka jana mpaka Februari mwaka huu Naibu Waziri Masauni alisema kwa nchi nzima ndani ya muda huo ni matukio nane tu huku akilipongeza jeshi la polisi kugundua na kudhibiti mianya ya uhalifu huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wafanyabiashara na wawekezaji walisifu juhudi zinazofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuwalinda hali inayowafanya wafanye shughuli zao kwa amani na usalama.