*****************************
NA EMMANUEL MBATILO
Katika mafanikio waliyoyapata Kurugenzi ya Ubunifu na Ujasiriamali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika mwaka wa fedha unaoisha, Chuo hicho kimedhamiria kuongeza fungu ili kuwapa nafasi watu wengi zaidi kuendeleza shughuli zao za utafiti na ubunifu.
Ameyasema hayo leo Makamu Msaidizi wa Masuala ya Uvumbuzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDIEC),Dkt.Amelia Buriyo katika mkutano na Wanahabari Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Wanahabari Chuoni hapo, Dkt.Amelia amesema kuwa baada ya Chuo hicho kufanya mabadiliko katika vitengo vyake ambapo shughuli za ubunifu na ujasiriamali zilikuwepo hapo awali zikaratibiw kwenye vitengo tofauti (IPI na UDEC) ziliwekwa chini ya uratibu wa pamoja ili kuongeza ufanisi katika kutoa huduma zake kwa fani muhimu katika ulimwengu wa sasa.
“Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika mwaka huu wa fedha unamalizika kilitenga kiasi cha sh. Bilioni Moja kwa shuguli za utafiti na ubunifu kwa Kampasi Kuu ya Julius Nyerere Mlimani na Milioni 400 Vyuo vyake shiriki vya MUCE na DUCE”. Amesema Dkt.Amelia.
Aidha Dkt.Amelia amesema kuwa katika miaka 4 ya utendaji wa kurugenzi hiyo kumekuwepo na mafanikio ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ari ya kusoma kozi ya ubunifu na ujasiriamali kwenye fani nyingi hapo Chuo.
Pamoja na hayo Dkt.Amelia amesema kuwa kuna wanafunzi ambao wanaendesha mradi wa SmartClass ambao wameingia fainali ya mashindano ya ubunifu ya jumuiya ya madola wamekuwa nao katika program hiyo ya uatamizi tangu Januari 2019.
“Katika kipindi cha mwaka mmoja huu ambao wamekuwa katika program ya uatamizi wameshiriki katika mashindano kadhaa yanayoandaliwa na kurugenzi yetu na wameshinda mara mbili. Tunajivunia vijana hawa jinsi wanavyotumia fursa hii ya uatamizi vizuri na hatua walioifikia”. Amesema Dkt.Amelia.
Kwa uapnde wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mradi wa SmartClass Bw.Salvatory Kessy amesema kuwa Smart Class imefanikiwa kuorodhesha miongoni mwa biashara 16 duniani kote zinazoleta mchango mkubwa katika maendeleo.
“Mashindano haya yalihusisha biashara zaidi ya 500 kutoka duniani kote.Jumuiya ya madola ikaichagua SmartClass kua miongoni mwa vumbizi nzuri na chache sana duniani zinazobadilisha maisha ya watu hapa Tanzania na barani Afrika”.
Nae Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Masuala ya Mipango SmartClass Bw.Adam Duma amesema kuwa mradi huo inatoa ajira kwa watu wenye ujuzi mbalimbali na mpaka sasa walimu zaidi ya 5,000 wa mambo mbalimbali kama vile masomo ya darasani, michezo, biashara, lugha, muziki , mambo ya teknologia na kilimo wamejisajili ndani ya mtandao wa SmartClass.
“Kupitia mradi huu, walimu hawa wanakuza kipato chao kwa kuwafundisha wanafunzi.Hii itawasaidia walimu kuimarisha hali zao za kimaisha”. Amesema Duma.
Duma amesema kuwa pamoja na mafanikio yao bado wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosa wawekezaji w hapa Tanzania na pia kutoka sehemu zingine dunianiwanaotaka kuwekeza katika biashara ndogo ambazo zinaweza kukua ndani ya miaka mitano ijayo.
SmartClass inapatikana katika mitandao ya kijamii kama vile instagram:smartclasstz, Twitter:smartclasstz, Facebook:smartclasstz na pia unaweza kutembelea tovuti yao www.smartclasstz.com.