Msanii Shetta akiimba na kucheza na baadhi ya wanafunzi katika viwanja vya Kashaulili katika Manispaa ya Mpanda
Mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Homera akizungumza na wananchi katika uzinduzi wa wiki ya kutokomea unyanyasaji wa kijinsia
………………………………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Katavi
Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa inayotajwa kuwa na idadi kubwa ya matukio ya unyanyasaji wa kijinsia ikiwa ni pamoja na utelekezaji wa familia
Akizungumza mara baada ya kuzindua wiki ya kupinga ukatili wa kijinsia katika kuelekea siku ya wanawake duniani iliyofanyika kitaifa katika manispaa ya Mpanda mkoani Katavi; Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera alisema wanaendelea kushughulikia mashauri mbalimbali
“Katika kuiunga mkono Wizara ya Afya, tumeshiriki katika ktatua kesi 314 za unyanyasaji wa kijinsia; kesi 100 za watoto waliotelekezwa, kesi 100 za wanawake waliotelekezwa na kesi 14 za wanaume waliotelekezwa” alisema Homera
Aidha Homera aliongeza kuwa katika kesi hizo wamepata mafanikio kwa kusuluhisha kesi 250 za ndoa ambazo zimesaidia wahusika wameweza kurudiana
Bi. Neema Kimei ni Msimamizi wa Haki za Binadamu katika taasisi ya kisheria Mkombozi Paralegal Organization iliyoko mkoani Katavi; alisema wamekuwa wakipokea mashauri mengi hasa ya wanawake kudhulumiwa mali na vipigo kwa wanandoa
Akitoa taarifa kwa niaba ya Katibu Mkuu; Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi Imelda-Evelyne Kamugisha alisema serikali imeendelea kutekeleza mpango wa kutokomeza ukatili wa kijinsia ambapo imeongeza madawati ya jinsia katika vituo vya polisi kufikia 420 na vituo vya mkono kwa mkono kutoka vituo 10 mwaka 2017 hadi vituo 13 mwaka 2019
Aidha uzinduzi huo wa wiki ya kutokomeza ukatili wa kijinsia uliambatana na msanii wa muziki wa kizazi kipya Nurdin Bilal Ally maarufu kama Shetta ambaye amewasihi watoto kuwa makini na watu wenye nia ovu
“Ukipewa chipsi za bure kataa, ukipewa pipi kataa, ukiahidiwa pesa za bure kataa” alisema Shetta wakati akizungumza na wanafunzi mbalimbali waliohudhuria uzinduzi huo katika viwanja vya Kashaulili katika Manispaa ya Mpanda