Baada ya jana madiwani 11 wa Jiji la Mbeya wakiongozwa na Mstahiki Meya, David Mwashilindi kuihama Chadema na kuhamia CCM, leo tena Diwani kutoka Kata ya Hunyari iliyopo Halmashauri ya Bunda mkoani Mara ametangaza kuhama Chadema na kuhamia CCM.
Makina Josephat ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Bunda na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama hiko kikuu cha upinzani ametangaza uamuzi wake huo leo jijini Dodoma na kupokelewa na MNEC wa CCM, Ismail Jamaa.
Akizungumza baada ya kumpokea Diwani huyo, MNEC Jamaa amesema wamempokea kiongozi huyo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa na kwamba taratibu zingine za kumpokea zitafanyika wilayani Bunda ambapo anaishi.
” Msururu wa wapinzani wanaojiunga na chama chetu unazidi kuongezeka kila siku, hii ni kwa sababu serikali ambayo ni ya CCM imefanya kazi kubwa ya kuwahudumia wananchi jambo ambalo wenye akili hawataki kupitwa nalo kwa kubaki upinzani,” Amesema Jamaa.
Nae Makina amesema kwa miaka minne ambayo Rais Dk John Magufuli ameongoza amegusa kila sekta na kumaliza ajenda zote ambazo wapinzani walikua wakizipigania hivyo haoni haja tena ya kuendelea kuwepo upinzani.
” Kwanini nibaki upinzani? Hili swali nimejiuliza sana kwa sababu Rais Magufuli amefanya kila ambalo nilitamani wananchi wafanyiwe. Huyu ni kiongozi wa mfano ambaye inabidi tumuunge mkono na siyo kumpinga kila siku.
Mazingira ya ufanyaji kazi upinzani ni magumu sana, nimeona nije CCM niweze kuwatumikia watu wa Bunda kwa nguvu na kasi ambayo Rais wetu amekua nayo kwa muda wote tangu aingie madarakani,” Amesema Makina.