Home Mchanganyiko NDITIYE: NUNUENI VIPURI KUKARABATI VICHWA VYA TRENI KWA WAKATI

NDITIYE: NUNUENI VIPURI KUKARABATI VICHWA VYA TRENI KWA WAKATI

0

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (aliyetangulia mbele katikati) akipata maelezo kuhusu ukarabati wa vichwa vya treni kutoka kwa Kelvin Kimario (wa kwanza kulia mbele), Meneja Msaidizi wa Karakana ya Reli, Morogoro wakati wa ziara yake kwenye Karakana hiyo

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa nne kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mhandisi Albert Magandi, Mkurugenzi wa Uhandisi Mitambo kuhusu utendaji kazi wa Karakana ya Reli, Morogoro wakati wa ziara yake kwenye Karakana hiyo

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) akipata maelezo kuhusu utengenezaji wa vichwa vipya vya treni kutoka kwa Mhandisi Wenceslaus Kamugisha, Meneja wa Mradi wa Kampuni ya SMH RAIL ya Malaysia wakati wa ziara yake kwenye Karakana ya Reli, Morogoro

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akisisitiza jambo kwa viongozi wa Karakana ya Reli, Morogoro wakati wa ziara yake kwenye Karakana hiyo

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kulia) akipata maelezo kuhusu ukarabati wa vichwa vya treni kutoka kwa Mhandisi Edgar Bakuza, Meneja wa Karakana ya Reli, Morogoro wakati wa ziara yake kwenye Karakana hiyo

Mafundi wa Karakana ya Reli, Morogoro wakiendelea kukarabati vipuri vya vichwa vya treni wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani) kwenye Karakana hiyo

…………………………………………………………………………………………………………

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amelielekeza Shirika la Reli Tanzania (TRC) kununua vipuri kwa ajili ya kufanya matengenezo na ukarabati wa vichwa vya treni kwa wakati

Nditiye ameyasema hayo wakati wa ziara yake jana kwenye Karakana ya Reli Morogoro ambapo alikagua matengenezo na ukarabati wa vichwa vya treni yanayoendelea kufanyika kwenye karakana hiyo mkoani Morogoro 

Pia, ameshuhudia utengenezaji wa vichwa vipya saba vya treni unaofanywa na Kampuni ya SMH Rail ya kutoka nchini Malaysia kwa kushirikiana na mafundi na wataalamu watanzania wa karakana hiyo 

Wakati akiwa ziarani hapo alifanya kikao na viongozi na mafundi wa Karakana hiyo na kubaini kuwa TRC inachukua muda mrefu kufanya manunuzi ya vipuri au oil kwa ajili ya kukamilisha ukarabati au matengenezo ya vichwa vya treni ambapo manunuzi yanachukua muda mrefu 

“wataalamu wa manunuzi wa TRC muache tabia ya kuchukua muda mrefu kufanya manunuzi ya vipuri au oil kwa ajili ya kufanya matengenezzo au ukarabati wa vichwa vya treni, kama kuna changamoto kwenye manunuzi au malipo, menejimenti ya TRC fanyieni kazi jambo hili,” alisisitiza Nditiye

Aliongeza kuwa hatuhitaji tutafute vipuri izidi miezi mitatu na fundi anaomba oil ili afanye matengenezo ya kichwa cha treni inachukua miezi miwili kwa kuwa sisi Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeona umuhimu wa reli, tutalinda reli yetu na tutaendelea kurekebisha njia ili reli iendelee kuchagiza uchumi na kuongeza pato la taifa letu kwa kuwa bila reli kichwa cha treni hakisogei na bila reli uchumi haupandi

Tunashukuru kwenye karakana hii tuna mafundi na wataalamu wa kutosha ambao wako tayari kufanya kazi kwa bidii na kujitolea ili kuhakikisha kuwa treni zetu zinatembea na reli yetu inafanya kazi na wako tayari kufundisha vijana ili waweze kuwaridhisha utaalamu huo

Naye Meneja wa Matengenezo ya Vichwa vya Treni, Karakana ya Reli ya Morogoro, Mhandisi Edgar Bakuza amekiri kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa vipuri kwa wakati kwa ajili ya kufanya matengenezo na ukarabati wa vichwa vya treni kwenye Karakana hiyo

“Ni kweli changamoto za vipuri ni kubwa, tunajitahidi kupambana nayo ndiyo maana tupo hapa kwa ajili ya kuzikabili changamoto ambazo zinatukabili na natumai kutokana na mashirikiano mazuri ambayo tunayo kati yetu sisi na viongozi wetu wa juu changamoto hizo zinafanyiwa kazi na natumai mwisho wa siku sisi hapa Morogoro huwa tunapimwa kutokana na uimara wa kazi tunazozifanya hasa katika hivi vichwa vya treni, uimara wake pamoja na uwingi wao katika hii fleet yetu ya locomotives katika hii reli ya kati, kwa hiyo tuko mbioni kuikabili na kuiondoa kabisa,” amefafanua Mhandisi Bakuza

Mhandisi Bakuza amesema kuwa wanaendelea na matengenezo ya vichwa saba vya kupangia mabehewa na mradi unaendelea vizuri na upo katika hatua nzuri ya kuweza kuukamilisha na sasa kazi ya kuendelea kuunga vyuma na mabati mbali mbali inaendelea ili kuweza kupokea vifaa mbali mbali ambavyo vimeagizwa nje ya nchi na tayari vifaa vingi vimefika kwenye Karakana hiyo, vifaa vingine vimeagizwa, vimesafirishwa na tayari vipo bandarini Dar es Salaam kwa ajili ya kugombolewa na kufikishwa Morogoro 

Ameongeza kuwa mradi huu utakapokamilika utawezesha kuondoa vichwa vikubwa vya treni kutoka katika kazi ya kupangia mabehewa ili vitumike katika kazi ya kuvuta mzigo mkubwa kwenda mikoa ya bara

Vichwa vinavyotengenezwa vitakuwa na kazi ya kuvuta mzigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam ili kuufikisha Bandari ya TRC iliyopo eneo la Kwala mkoani Pwani ili mabehewa hayo yavutwe na kichwa kikubwa cha treni kuelekea bara

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa TRC, Halima Lumuli alikiri uwepo wa changamoto hiyo ya upatikanaji wa vipuri ila watajitahidi kuhakikisha vinapatikana kwa kuwa vichwa vya treni ndio kila kitu katika utendaji wa TRC na Shirika litajitahidi kuboresha eneo hilo pamoja na kuboresha maslahi ya watumishi na kuwapatia mafundi mafunzo ya kuongeza uwezo na weledi ili utendaji kazi wao uweze kuongeza mapato ya Shirika