*****************************
MWAMVUA MWINYI,PWANI
MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoani Pwani Zaynab Vullu, amekabidhi vifaa tiba katika zahanati za Kikongo na Disunyara, Kibaha Vijijini lengo ni kuwapunguzia changamoto wagonjwa wanaopatiwa tiba kwenye zahanati hizo.
Akizungumza kwenye zahanati ya Kikongo kabla ya kukabidhi vifaa hivyo ikiwemo mashuka, vipomo vya presha, sukari, apron za kuvaa kifuani na mipira ya kitanda ya kuzuia shuka zisichafuke, Vulu amesema kuwa kwa uchache wake ameamua kufika hapo kukabidhi vifaa tiba hivyo.
Pamoja na hayo, Vullu amekitembelea kikundi cha Umoja ni Nguvu kilichopo Kikongo, ambacho amekikabidhi cherehani moja na jora la kitambaa kitachotumika kuwashonea sketi na kaptura wanafunzi 70 wanaoishi kwenye mazingira hatarishi wakisaidiwa na kikundi hicho.
Alisema,ametoa misaada hiyo kutokana na kuguswa na changamoto hizo ili kupunguza upungufu uliopo.
“Nilishakuja kukabidhi tenki hili la maji, leo nawakabidhi vifaa hivi vichache ambavyo nina imani vitatusaidia katika kuwapatia huduma wananchi wetu,” alisema Vulu.
Pia zahanati ya Kilangalanga, ambapo mganga Mkuu wa zahanati hiyo Raya Mohamed alishukuru na kutaja changamoto nyingine ya vipimo vya presha na kisukari vimeharibika.
Akizungumza na wanakikundi wa Umoja ni Nguvu kabla ya kuwakabidhi cherehani na jora la kitambaa, Vullu alisema , amefika baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mbunge wa jimbo hilo Humoud Jumaa, alipokuwa kwenye hafla ya kumaliza mzunguko wa mwaka, ambapo alitoa ahadi za wabunge watatu wa Viti Maalumu.