Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akisikiliza hoja na malalamiko kutoka kwa mmoja wadau wa sekta ya uvuvi katika Kijiji cha Kigombe Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga.
Mbunge wa Jimbo la Pangani Mhe. Jumaa Aweso ( wa kwanza kutoka kulia) akifuatiwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega wakikagua punda waliyopo katika Shamba la Serikali Mivumoni Wilaya ya Pangani Mk.
Baadhi ya wadau wa sekta ya uvuvi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega wakati akizungumza nao kwenye kikao kilichofanyika Kijiji cha Kigombe kilichopo Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga.
………………………………………………………………………………………………..
Serikali imewataka maafisa uvuvi nchini kusimamia vyema sheria, kanuni na taratibu katika sekta ya uvuvi nchini bila kuwaonea wadau wa sekta hiyo ili iongeze tija zaidi kwa wadau hao.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amebainisha hayo wakati wa siku ya kwanza ya ziara yake Mkoani Tanga, Alhamisi wiki hii (20.02.2020), kwa kutembelea Wilaya za Muheza na Pangani kwa lengo la kusikiliza maoni, kero na maswali kutoka kwa wadau ambapo amebaini changamoto kadhaa zikiwemo za wavuvi kutopatiwa taarifa na elimu sahihi juu ya sekta hiyo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
“Maafisa uvuvi ninawaagiza hakikisheni mnasimamia sheria, na pia mtende haki, msimuonee mtu yeyote na watakaobainika na kujihusisha na vitendo vya rushwa tutawachukulia hatua za kisheria.” amesema Mhe. Ulega wakati akizungumza na wadau wa sekta ya uvuvi katika Kijiji cha Kigombe kilichopo Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Pangani Mhe. Jumaa Aweso ambaye ameshiriki katika kikao hicho amemuomba Mhe. Ulega kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wavuvi zikiwemo za kupatiwa elimu juu ya sekta hiyo.
Akiwa katika kijiji cha Pangani Mashariki katika Wilaya ya Pangani alipotembelea Shamba la Serikali la Mivumoni Naibu Waziri Ulega amewataka wafugaji kutovamia mashamba ya serikali kwani kwa kufanya hivyo ni uvunjifu wa sheria na badala yake wafuate taratibu wanapohitaji maeneo kwa ajili ya malisho ya mifugo yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika siku ya kwanza ya ziara yake kwenye mikutano wilaya za Muheza na Pangani Mkoani Tanga, baadhi ya wadau wa sekta ya uvuvi wamemuomba Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega kuwatatulia changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo zikiwemo za wingi wa tozo, mikopo na elimu ya vifaa sahihi vinavyotakiwa katika shughuli za uvuvi ili kujiepusha na vitendo vya uvuvi haramu bila kukusudia.