Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu akiongea na wadau katika kikao cha kukuza uelewa wa Sheria na Utekelezaji wa Kanuni ya Katazo la Mifuko ya Plastiki kwa Wazalishaji, waingizaji, wasambazaji na wauzaji wa Mifuko mbadala ya Plastiki. Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa LAPF, Jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha (kushoto) Ni Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samwel Gwamaka, Bi. Kemilembe Mutasa Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira na
Bw. Jabir Abdi Kaimu Mkurugenzi Mkuu Shirika la Viwango Tanzania.
Picha na Lulu Mussa
*****************************
NA EMMANUEL MBATILO
Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa raisi, muungano na mazingira Mussa Azzan Zungu amezitaka halmashauri zote nchi kuanza kutoa elimu ya mazingira kwa wananchi hususani kwenye matumizi ya mifuko mbadala.
Wito huo ameutoa leo jijini Dar es salaam katikati kikao cha wadau wa uzalishaji, uingizaji,usambazaji na uuzaji wa mifuko mbadala ya plastic ambapo amesema kuwa halmashauri kwa mujibu wa sheria wanaowajibu wakutoa elimu kwa wananchi juu ya udhibiti uchafuzi wa mazingira kwa njia mbalimbali.
Aidha amewataka wazalisha na wananchi kuacha kutumia Vifungashio vya plastiki kubebea mizigo na bidhaa mbalimbali ili kuhakikisha mazingira yanalindwa na kuendelea kuwa salama.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa baraza la usimamizi mazingira (NEMC) Prof.Samweli Mafwenga amesema mpaka sasa kuna viwanda 72 nchini ambavyo vinatengeneza mifuko mbadala ambapo vimetoa ajira kwa vijana 2761.
“Baadhi ya viwanda vya plastiki waliomba kupatiwa shehena ya plastiki iliyokusanywa ili waweze kuitumia kama malighafi ya kuzalisha bidhaa nyingine za plastiki ambazo hazijazuiwa.kama vile viwanda vya mabomba ya maji, chupa za plastiki na kadhalika”. Amesema Prof.Mafwenga.
Ameongeza kuwa mifugo mingi ilikuwa inaathirika kwa kula mifuko ya plastiki kwani wapo wafugaji waliotoa ushuhuda kupungua kwa vifo vya mifugo katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha amewataka wananchi kutoa taarifa kwa wanaokiuka sheria kwani mpaka sasa kuna muitikio mdogo kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu kukiukwa sheria za katazo la mifuko ya plastiki.