Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi Biashara Ndogo na za Kati, Filbert Mponzi (katikati) akiwa na Kamishna wa Bima kutoka Mamlaka ya Bima nchini (TIRA), Dkt. Mussa Juma (kushoto) wakati wa uzinduzi wa NMB Bancassurance uliofanyika jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja Mwandamizi wa Bima NMB – Martin Massawe.
Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi, Biashara Ndogo na za Kati – Filbert Mponzi akiongea kabla ya kuzindua huduma ya NMB Bancassurance jijini Dar es Salaam.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Bi. Margaret Ikongo akipongezana na Kamishna wa Bima kutoka Mamlaka ya Bima nchini (TIRA), Dkt. Mussa Juma baada ya kuzindua, NMB Bancassurance jijini Dar es Salaam. Katikati ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi, Biashara Ndogo na za Kati – Filbert Mponzi.
Afisa Mkuu wa wateja Binafsi, Biashara ndogo na za kati, Filbert Mponzi (kushoto) na Kamishna wa Bima kutoka katika Mamlaka ya Bima nchini (TIRA), Dkt. Mussa Juma wakizindua NMB Bancassurance. Katikati ni Meneja wa usimaimizi wa Fedha B.o.T, Mussa Sadat.
……………………………………………………………………………………………………………..
Benki ya NMB imeanza kutoa huduma za bima katika matawi yake yote 224 nchini kote.Huduma hii imefuatia uzinduzi wa huduma ya bima kupitia benki (Bancassurance) uliofanyika jana jioni jiji Dar es Salaam.
Huduma za bima zitakazopatikana katika matawi ya Benki ya NMB ni pamoja na zile za kampuni za Sanlam Life, UAP, Shirika la Bima la Taifa (National Insurance Corporation – NIC), Jubilee, Shirika la Bima la Zanzibar (Zanzibar Insurance Corporation – ZIC) na Reliance.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja Mwandamizi wa Bima wa Benki ya NMB, Bw. Martin Massawe, alisema uwepo wa matawi ya benki yake katika wilaya zote nchini kutasaidia kukuza sekta ndogo ya bima na kuinua mchango wake katika pato la taifa.
“Tulipata leseni ya kutoa huduma za bima mara baada ya kupitishwa kwa kanuni za Bancassurance mwaka jana. Kutokana na kupatikana kwa matawi yetu katika wilaya zote nchini, tunaamini kupatikana kwa huduma za bima katika matawi yetu kutasaidia kukuza sekta ndogo ya bima,” alisema.
Naye Kamishna wa Bima wa Mamlaka ya Bima nchini (TIRA), Dkt. Mussa Juma alisema serikali kupitia taasisi yake inachukua juhudi mbali mbali ili kukuza sekta ndogo ya bima nchini ili mchango wake katika pato la taifa ufikie asilimia tatu ifikapo mwaka 2023.
Hivi sasa sekta ndogo ya bima zinazosimamiwa na Mamlaka ya Bima Nchini, huchangia asilimia 0.7 ya pato a taifa.“Malengo yetu ni kuhakikisha kuwa asilimia 60 ya Watanzania watu wazima wawe wanapata huduma za bima ifikapo mwaka 2024. Tunalenga pia kuhakikisha kuwa asilimia 60 ya watanzania wote wawe wameweza kuelewa umuhimu wa bima ifikapo mwaka 2024,” alisema.
Ili kufikia azma hiyo, kampuni za bima, madalali wa bima, mawakala wa bima na benki zinazotoa huduma za bima (Bancassurance) zitalazimika kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa Watanzania ili wapate kuelewa umuhimu wa kuziwekea bima mali zao.
Alisema wadau wa bima watalazimika kutumia teknolojia mpya ili kuwafikia watu wengi zaidi, wakiwemo wafanyabiashara ndogo ndogo na baba/mama lishe.
Naye Afisa Mkuu wa wateja binafsi, Biashara Ndogo na za Kati wa Benki ya NMB – Filbert Mponzi alisema benki hiyo imeshatoa elimu ya bima kwa wafanyakazi wake wapatao 200 ambao wamethibitishwa kumudu utoaji wa huduma za bima kwa wateja.
“Tunaamini ujio wa Benki ya NMB katika kutoa huduma za bima ni ‘game changer’ (ibadili mwenendo wa sekta) na kuipeleka sekta katika viwango vya juu,” alisema.
Alisema NMB itatumia uwepo wa vilabu vya kibiashara katika maeneo mbali mbali nchini ili kueneza ujumbe wa umuhimu wa bima. NMB Business Club ni mahali muafaka pa kuelimisha wafanyabiashara juu ya masuala mbalimbali kuhusu biashara zao. Vilabu vya kibiashara vya NMB vimezinduliwa nchini kote kwa lengo la kutatua changamoto zinazo wakabili wafanyabiashara nchini.
Benki pia itakuwa ikikusanya maoni ya aina za bima zinazohitajika katika maeneo mbali mbali kulingana na mahitaji ya wateja na kuyapeleka katika kampuni za bima.
Wakati kukiwa na hofu miongoni mwa baadhi ya watu wa bima kuwa ujio wa Bancassurance utawaondoa sokoni madalali na mawakala wa bima, Dk Juma anaamini huduma hiyo mpya (Bancassurance) itaisaidia kuongeza wigo wa sehemu za watu kwenda kupata huduma za bima.