************************************
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo February 18 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uturuki Nchini Tanzania Mhe. Ali Davulaglu, Balozi wa Tanzania Nchini Uturuki Prof.Elizabeth Kiondo, Mstahiki Meya kutoka Uturuki, Wawekezaji na Wafanyabiashara zaidi ya 40 kutoka Nchini Uturuki waliokuja Kutazama na kuchangamkia fursa za Uwekezaji wa Viwanda jijini Dar es salaam.
Katika Mazungumzo hayo RC Makonda amewahakikishia Wawekezaji hao kuwa Serikali ya Mkoa huo itawapatia ushirikiano wa kutosha wawekezaji wote wanaotaka kuwekeza ili kutimiza malengo ya Rais Dkt. John Magufuli ya Tanzania ya Viwanda.
Aidha RC Makonda amewaeleza wawekezaji hao kuwa Jiji hilo linajivunia kuwa na Amani na Utulivu pamoja na fursa ya uwepo wa Bandari, Uwanja wa Ndege pamoja na Miundombinu yote muhimu ya kuvutia Uwekezaji.
Hata hivyo RC Makonda amesema February 20 atawapeleka wawekezaji hao Wilaya ya Kigamboni ili wakajionee maeneo yaliyotengwa kwaajili ya Uwekezaji wa Viwanda huku akimshukuru Balozi wa Tanzania Nchini Uturuki Prof. Elizabeth Kiondo kwa kuwaleta wawekezaji hao.
Nae Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Mhe. Ali Davutaglu amemuhakikishia RC Makonda kuwa Uturuki itazidi kuendeleza uhusiano na ushirikiano na Tanzania katika nyanya mbalimbali za maendeleo na wamemualika RC Makonda kwenda kutembelea Nchi ya Uturuki.