Home Makala VIWANJA VIKIWA BORA

VIWANJA VIKIWA BORA

0

******************************

SHAIRI

1. Kushukuru ni kikoa, kwa sisi Watanzania,
Ya wageni sitatoa, kwani sijayasikia,
Kwa hili nimejinoa, nipate kushabikia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

2. Azam wametutoa, kimasomaso sikia,
Runinga zimeondoa, maneno ya kusikia,
Timu ile inaloa, twaona si dhahania,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

3. Tafiti ninayotoa, siyo ya kufikiria,
Runinga imetoboa, wapi tunapotitia,
Naamini sitaboa, hebu yangu fwatilia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

4. Siku nyingi nasogoa, mechi zinapoishia,
Mengi wanayoyatoa, siyo ya kushangilia,
Ya marefa kiondoa, viwanja wanitajia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

5. Jua sisi twajitoa, tupate kufurahia,
Wachezaji wakitoa, pasi ziweze vutia,
Siyo kama wachokoa, shamba la bibi Asia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

6. Darisalamu ondoa, na Bukoba nayo pia,
Ukicheza watoboa, viwanja vinavutia,
Pasi wanazozitoa, wachezaji twaringia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

7. Simba Yanga wakohoa, timu zinapowajia,
Vijana wanajitoa, kwa soka lilotulia,
Wakongwe jasho waloa, wapenzi wajinamia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

8. Alliance kiwatoa, Lipuli watakujia,
Kwa Mwadui utaloa, uzungushwe kama pia,
Mtibwa watazizoa, pointi uzowania,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

9. Namungo walijitoa, Simba kuwashambulia,
Walicheza bila doa, kama ni Naijeria,
Kama VARI tungetoa, tatu isingeingia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

10. Wagosi sijawatoa, na Magereza sikia,
Hata timu za Kondoa, Ligi zingeifikia,
Maisha ngekua poa, na pesa zingeingia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

11. Gwambina wamejitoa, kiwanja kutuchangia,
Haya mambo ya kikoa, ni bora kushangilia,
Upweke kimeondoa, wachezaji wasifia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

12. Maneno haya natoa, Gama nikimlilia,
Vile alivyojitoa, viwanja kutufanzia,
Hatuwezi mpopoa, amani twamswalia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

13. Viongozi wa mikoa, ujumbe nawatumia,
Na wilaya za mikoa, Madisii mwasikia,
Angalau kwa mkoa, kiwanja hebu anzia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

14. Mpira unao boa, viwanja vinachangia,
Tunabaki kusogoa, timu zatuchafulia,
Kumbe tukikokotoa, ni viwanja vimevia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

15. Azam mmetutoa, kimasomaso sikia,
Uwanja mmeutoa, twacheza kifamilia,
Kimataifa ni poa, pongezi zangu sikia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

16. Simba mnajiondoa, kwa wale walofulia,
Bunju imekua poa, mazoezi mwafanyia,
Ongezeni kujitoa, uwanja kujifanyia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

17. Yanga kama ni madoa, hayo mmejifutia,
Muendako sasa poa, nasi twawafwatilia,
Usasa tawaokoa, ujima ukiishia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

18. Jeshi mfano natoa, jinsi nawaaminia,
Mwaweza mkatutoa, kama mkishapania,
Uwanja mkatoboa, popote palipo njia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

19. Viwanja mkichongoa, pesa zitawavamia,
Ajira mtazitoa, njaa hatutasikia,
Makato mliyokitoa, kidogo yatabakia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

20. Samatta ametutoa, tunatamba Tanzania,
Hata pesa akizoa, zitakuja Tanzania,
Akiwekeza tatoa, mchango kwa Tanzania,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

21. Msuva sijamwondoa, aijenga Tanzania,
Ulimwengu kokotoa, faida kwa Tanzania,
Viwanja tukitotoa, ni uchumi Tanzania,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

22. Maoni haya natoa, yasiishie kwa njia,
Yawafikie watoa, maamuzi yenye nia,
Wasije niweka doa, kwamba nawafwatilia,
Viwanja vikiwa bora, kina Samatta ni wengi.

Na Lwaga Mwambande
© Kila Mwenye Pumzi Amsifu Bwana (KimPAB) 2020