Home Mchanganyiko MHE.SIMA AMEWATAKA WACHIMBAJI WADOGO KUHIFADHI MAZINGIRA

MHE.SIMA AMEWATAKA WACHIMBAJI WADOGO KUHIFADHI MAZINGIRA

0

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima akizungumza na wachimbaji wadogo wa Sekenke 1 wilayani Iramba mkoani Singida alipofanya ziara ya kukagua namna wanavyohifadhi mazingira katika shughuli zao pamoja na kutoa elimu kuhusu madhara yanayoweza kutokea katika matumizi ya zebaki kwenye uchenjuaji wa dhahabu.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima (wa tatu kulia mwenye Kaunda suti) akipata maelezo kuhusu mchakato wa
uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu kutoka kwa mmoja wa viongozi wa wachimbaji wadogo wa Sekenke 1 wilayani Iramba mkoani Singida alipofanya ziara ya kukagua namna wanavyohifadhi mazingira katika shughuli zao.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima akiangalia miti inayotumiwa na wachimbaji alipotembelea wachimbaji wa machimbo ya Sekenke ambayo inatumiwa kuimarisha mashimo wanayochimba ambapo alitumia ziara yake kusisitiza pia upandaji miti ili kuhifadhi mazingira.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima akisaini kitabu cha wageni alipowasili machimbo ya Sekenke 1 wilayani Iramba mkoani Singida.

******************************

Na Robert Hokororo, Singida

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima amewataka wachimbaji wadogo kuhifadhi mazingira katika maeneo yao ya
machimbo kwa kupanda miti.

Sima alitoa kauli hiyo akiwa katika ziara yake ya kutembelea wachimbaji wa  machimbo ya Sekenke 1 wilayani Iramba mkoani Singida ikiwa ni sehemu ya
ziara yake mkoani humo.

 

Katika ziara hiyo ya kuangalia namna wachimbaji hao wanavyotunza mazingira pamoja na kuwapa elimu kuhusu madhara ya matumizi ya kemikali ya zebaki alisema ni wajibu kwao kuhakikisha hawakati miti ovyo ili kuepusha changamoto za kimazingira.

 

Sima alisema Serikali inatambua mchango wa wachimbaji wadogo hapa nchini na ndio maana imeridhia Mkataba wa Minamata kuhusu matumizi ya zebaki na kuwa pamoja na hatua hiyo lakini pia inasisitiza upandaji miti na kutunza
mazingira na kuwa ni jukumu la Serikali kuhakikisha uchimbaji unakuwa salama kwa mazingira.

 

“Maisha yetu yanategemea mazingira safi na salama lakini wakati tunaendelea kutembea katika eneo hili tumeona miti ni michache, kiafya hii si salama niwaombe mwakilishi wa Mkurugenzi, mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya kwa
kushirikiana na watu wa madini eneo hili lipandwe miti ya kutosha ili tutunze mazingira,” aliagiza.

 

Aidha naibu waziri huyo aliwataka wachimbaji hao kutafuta mbadala wa matumizi ya miti ambayo wanakata kwa ajili ya kuimarisha mashimo wakati wanafanya
shughuli za uchimbaji.

 

Kwa upande mwingine Sima alisema kuwa Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki ulioridhiwa na Tanzania hivi karibuni una kipengele kinachosisitiza uanzishwaji wa vikundi vya wachimbaji.

 

Alisema hatua ya kuanzisha vikundi itarahisisha ukopeshaji kwa urahisi kupitia taasisi za fedha zikiwemo benki hapa nchini kuliko ambavyo inavyokuwa kwa
mmoja mmoja.

 

“Ndugu zangu ni wakati sahihi ambapo Rais kwa adhamira yake ya kuhakikisha wachimbaji wadogo wanalindwa na tumepokea kodi alizoondoa sasa tupokee namna anavyolinda afya zetu,” alisema.

 

Kwa upande wake Afisa Mazingira wa Mkoa wa Singida Charles Kidua alisema kuwa takriban hekta laki nne za misitu hupotea kila mwaka kutokana na changamogto ya ukataji.

 

Kidua alifafanua kwa kusema kuwa ili kuepusha nchi yetu kugeuka jangwa, Serikali imekuwa ikiendelea kuwataka wananchi wapande miti kwa wingi badala ya kukata.