Wajumbe wa Kamati ya Michezo ya mashindano ya Mei Mosi wakiwa kwenye kikao cha Kwanza cha maandalizi ya michezo hiyo kilichofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro.
Katibu Mkuu wa Kamati ya Michezo ya mashindano ya Mei Mosi, Moshi Makuka (aliyenyoosha mikono) akisisitiza jambo kwenye kikao cha Kwanza cha maandalizi ya michezo hiyo kilichofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Mkoani Morogoro.
Wajumbe wa mkutano wa maandalizi wa michezo ya mashindano ya Mei Mosi (pichani) wakiwa kwenye kikao cha maandalizi ya michezo hiyo kilichofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), mkoani Morogoro
………………………………………………………………………………………………..
Na Bahati Mollel, Morogoro
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania (Takukuru) mkoa wa Mwanza itashirikishwa kwenye michezo ya mashindano ya Mei Mosi inayotarajiwa kuanza Aprili 16-29, 2020 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, endapo kutakuwa na timu za Wizara, taasisi za Umma na Binafsi zitawatumia wachezaji wasiokuwa watumishi wao halali.
Katibu wa Kamati ya michezo hiyo, Moshi Makuka, alisema hayo mwishoni mwa wiki kwenye kikao cha kwanza cha maandalizi ya michezo hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Morogoro, ambapo suala hilo limewekwa kwenye kanuni namba 13 kati ya 15 zilizopitishwa na wajumbe wote walioshiriki kwenye kikao hicho.
Makuka alisema mbali na Takukuru kushirikishwa kubaini uhalali wa mchezaji aliyesajiliwa na timu iliyomchezesha, pia viongozi wote walioshiriki kumsajili mchezaji huyo wataripotiwa kwenye taasisi hiyo, ili sheria za nchi zichukue mkondo wake.
“Haya mashindano yanajumuisha watumishi halali wa taasisi na wizara hivyo hairuhusiwi kuwachezesha wachezaji ambao sio watumishi halali, kwa lengo la kujipatia ushindi, hili ni katazo na kanuni yetu ipo wazi kabisa, hivyo timu zisithubutu kuja na wachezaji hao kabisa,” alisisitiza Makuka.
Alizitaja adhabu ambazo timu itakayobainika kumtumia mamluki ni pamoja na viongozi wake watafungiwa kushiriki michezo hiyo kwa muda wa miaka miwili na nakala ya barua itawasilishwa kwa Mwajiri wake; timu itatozwa faini ya Tshs. 500,000; timu husika itapokonywa ushindi endapo itakuwa imeshinda; timu itaondolewa kwenye mashindano.
Kamati imesema mamluki wanadhibitiwa kwa wanamichezo kuwa na vitambulisho halisi vya kazi, Kadi ya Bima ya Afya, Kadi ya Mfuko wa Jamii na hati ya Malipo ya mshahara za miezi miwili ‘salary slip’.
Hatahivyo, Makuka alisema tyimu zote shiriki zinatakiwa kuwahi mkoani Mwanza tarehe 14 Aprili, 2020 ambapo ndipo sherehe za Sikukuu za wafanyakazi zitafanyika Kitaifa kama ilivyotangazwa awali, ambapo timu itakayochelewa hadi tarehe 20 Aprili, 2020 itakuwa imejiondoa kwenye mashindano hayo.
“Timu ikichelewa inawapa shida na kuwaumiza wachezaji kwa kuwa watacheza mfululizo ili kwenda na ratiba, hadi kufikia michezo yao iliyosalia, hivyo hii hatutaki kwani michezo itakuwa haina ushindani kwa kuwa wachezaji wa timu moja watakuwa wamechoka kwa kucheza mfululizo wa mechi mbili au tatu kwa siku, hivi huu ni mwezi wa pili muanze kufuatilia ruhusa za wachezaji wenu,” alisema Makuka.
Kamati inategemea ushiriki wa timu zaidi ya 25, kwa kuwa zinaongezeka kila mwaka ambapo mwaka jana zilishiriki timu 23. Michezo itakayoshindaniwa ni pamoja na soka, netiboli, kuvuta kamba, baiskeli, riadha, karata, bao na draft.
Pia Makuka amesisitiza timu shiriki kulipa ada ya ushiriki kwa wakati, ili fedha hizo zitumike katika ulipaji wa gharama mbalimbali za uendeshaji wa mashindano hayo.
Ada ya ushiriki ni Tshs. 1,000,000 ambapo kila timu inatakiwa kulipa mapema kabla ya tarehe 6 Aprili, 2020, ili timu ziweze kupewa kadi za ushiriki zitakazofanikisha usajili wao.
Halikadhalika Makuka amesema timu zote zilizotwaa vikombe kwa kuwa washindi wa Kwanza hadi wa tatu wanatakiwa kurejesha vikombe walivyoshinda kabla yatarehe 29 Machi, 2020 na timu itakayochelewa utatozwa faini ya Tshs. 200,000.
Wakati huo huo, Makuka amesema timu zinaruhusiwa kushiriki kwenye michezo ya mashirikisho mbalimbali yakiwemo ya Shimiwi, Shimmuta na Mei Mosi, na sio kusubiri michezo ya shirikisho moja, ambayo kwa wakati huo inakuwa haijafanyika kwa sababu mbalimbali.