Mbunge wa jimbo la Ushetu, Mheshimiwa Elias Kwandikwa akizindua jengo la Chama cha Msingi cha Ushirika (Uyogo AMCOS) katika kata ya Uyogo na kuahidi mifuko ya saruji 100 kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo.
Mbunge wa jimbo la Ushetu, Mheshimiwa Elias Kwandikwa, akizungumza na wananchi wa kata ya Uyogo kuhusu maendeleo ya jimbo katika miradi inayoendelea kutekelezwa na ile iliyokamilika katika kata hiyo.
Mbunge wa jimbo la Ushetu, Mheshimiwa Elias Kwandikwa akikagua jengo la Chama cha Msingi cha Ushirika (Uyogo AMCOS) katika kata ya Uyogo kabla ya kulizindua.
Mbunge wa jimbo la Ushetu, Mheshimiwa Elias Kwandikwa, akiongea na wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Nsunga katika kata ya Uyogo iliyopo katika Halmashauri ya Ushetu.
Baadhi ya wananchi katika kata ya Uyogo wakimshangilia Mbunge wa jimbo la Ushetu, Mheshimiwa Elias Kwandiwa, (hayupo pichani).
Mbunge wa jimbo la Ushetu, Mheshimiwa Elias Kwandikwa, akizungumza na wananchi katika kijiji cha Nsunga kuhusu kazi za kimaendeleo zinazoendelea kufanyika katika kijiji hicho.
………………………………………………………………………………………………………
Mbunge wa jimbo la Ushetu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Elias Kwandikwa, amewataka wananchi kuepukana na vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikishamiri hususan katika vipindi vya uchaguzi ambapo wagombea wengi wamekuwa wakiwashawishi wananchi kwa kutoa rushwa ili waweze kuwachagua.
Aidha amewasisitiza wananchi wake kuendelea kufanya kazi kwa bidii hasa katika sekta ya kilimo, ufugaji na madini ili kuunga mkono jitihada za Serikali na kufikia malengo ya uchumi wa kati ifikapo 2025.
Wito huo ameutoa akiwa jimboni kwake kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Nsunga, Nsenai, na Uyogo katika kata ya Uyogo wilayani Kahama mkoani Shinyanga wakati akizungumzia maendeleo ya jimbo yaliyotekelezwa kwa kipindi cha miaka 4 tangu ulipofanyika uchaguzi mkuu Oktoba, 2015.
“Nasema hivi wale watu wanaokuja kudanganya kwa fedha wamenoa dafu Serikali inafanya kazi na hata nyie wenyewe mnaona tupo vizuri, kwa hiyo msidanganyike”, amesisitiza Mbunge huyo.
Aidha Mhe. Kwandikwa ameeleza kuwa kuelekea miaka 5 tangu wananchi wa jimbo hilo kumpa ridhaa ya kuwawakilisha wanapaswa kujivunia juu ya miradi iliyotekelezwa kwa kipindi hicho na ile inayoendelea.
Amebainisha baadhi ya miradi iliyotekelezwa jimboni hapo ikiwemo ya maji yenye visima virefu katika kata za Ukune, Mpunze, Chambo, Bulungwa na sabasabini, pia barabara zinazounganisha kata hadi kata, na usambazaji wa umeme kwa vijiji 56 ambao unatekelezwa kupitia REA na miradi mingine mingi kwa manufaa ya wananchi.
Wakizungumzia hotuba ya Mbunge huyo, baadhi ya wananchi wamempongeza kwa kuwa mtetetezi wa wanyonge ambaye amejitoa kuwapigania kwa kuonesha dira ya maendeleo inayoendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mbunge wa jimbo la Ushetu ameendelea na ziara yake ya kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika jimbo lake lenye kata 20 huku akiendelea kutatua kero za wananchi katika nyanja zote za Elimu, Kilimo, Umeme, Maji, Afya na Michezo.