Home Mchanganyiko DK KAWAMBWA AOMBA VIFAA TIBA KATIKA KITUO CHA AFYA MATIMBWA

DK KAWAMBWA AOMBA VIFAA TIBA KATIKA KITUO CHA AFYA MATIMBWA

0
 
…………………………………………………………………………………………………..
NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
MBUNGE wa Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa ameeleza kukamilika kwa kituo cha afya Matimbwa ni mkombozi kwa wakazi wa Yombo,Matimbwa na maeneo jirani ambao walikuwa wakitaabika kukosa huduma za afya karibu hasa huduma za uzazi na upasuaji.
Dkt Kawambwa alisema hayo katika mkutano maalumu uliotumika kwa ajili ya kukamilishwa kwa ahadi iliyotolewa  na Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Pwani Zaynab Vulu, ya mifuko 20 ya saruji na mbunge Kawambwa kutoa mifuko hiyo 10 kwa ajili ya umaliziaji wa wodi ya uzazi kijiji cha Yombo.
Alibainisha ,kwasasa hatua iliyopo ni kupelekwa kwa vifaa tiba katika kituo hicho cha afya na ameshafanya mawasiliano na Waziri wa TAMISEMI Suleiman Jafo, ili vifaa hivyo vipelekwe mapema wananchi waanze kunufaika na juhudi za kuboresha huduma za afya zilizofanyika .
“Nimezungumza na Jafo atupie jicho suala hili la kupatiwa vifaa jengo la uzazi na kituo hiki ili kianze kutoa huduma nzuri kama kituo cha Kerega,
“Nimeomba ingewezekana fedha za vifaa tiba ambazo zimeelekezwa katika vituo ambavyo havijakamilika ingeelekezwa hapa ambako kituo kipo tayari na baadae vituo hivyo vingine vitapatiwa fungu la hapa “alieleza.
Nae mbunge wa viti maalum mkoani Pwani, ZaynabMatitu Vulu alielezea kutokana na kazi kubwa iliyotekelezwa na serikali ,ameshawishika kuunga mkono juhudi hizo kwa kidogo alicho nacho.
Diwani wa Kata ya Yombo ,Mohamed Usinga akizungumzia pamoja na suala la nishati linavyotekelezwa katika kata hiyo ,alisema, wakati wa zoezi la uchimbaji wa mashimo kwa ajili ya kusimikwa nguzo, kuna kijana mmoja mkazi wa Kitongoji cha Chasimba amepatwa na tatizo la kupoteza sauti akiwa kazini lakini kwasasa anaendelea vizuri.
Hata hivyo,diwani huyo wa kata ya Yombo, alipongeza serikali kwa kazi kubwa inayondelea kuifanya na kusema ambae haoni kinachofanywa na serikali katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, miundombinu ya barabara, kilimo,nishati,uwekezaji na afya  basi atakuwa na matatizo yake binafsi.