*******************************
Na Daudi Manongi, MAELEZO
Mkutano wa kwanza wa kamati ya Mawaziri wanaohusika na Menejimenti ya Maafa kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utafanyika tarehe 18-21 Februari visiwani Zanzibar, 2020 ukiwa na lengo la kuchochea juhudi zilizopo katika kupunguza madhara ya maafa ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar, Mhe.Dkt. Ali Mohamed Shein.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Kazi,Ajira,Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma.
“Katika mkutano huu wa SADC tutajadiliana namna ya kuwekeza katika kupunguza madhara ya maafa kwa kuwa gharama za usimamizi wa maafa kama ya mafuriko huzilazimu nchi wanachama kuelekeze rasilimali zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo na badala yake huelekezwa katika shughuli za kurejesha hali”, aliongeza Waziri Mhagama
Ameongeza kuwa nchi wanachama ikiwemo Comoro, Malawi, Msumbiji na Zimbabwe kwa mwaka 2019 zilipata mafuriko yaliyosababishwa na vimbunga Idai na Keneth na gharama zake misaada na madhara zilikuwa kubwa sana zikikadiriwa kuwa dola bilioni 10.
Ili kwenda sambamba na juhudi za kikanda na kimataifa , Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli itaendelea kuimarisha uwezo wake wa usimamizi wa maafa katika Nyanja zote, aliongeza Mhagama.
“Tayari Serikali ya Awamu ya Tano imetunga Sheria ya Usimamizi wa Maafa ya Kitaifa na.7 ya 2015 na kanuni zake, tunao wasifu wa janga la mafuriko na ukame wa kitaifa na mkakati wa Taifa kupunguza madhara ya maafa”, aliongeza Waziri Mhagama.
Itakumbukwa kuwa Tanzania ilichukua rasmi nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya kuanzia mwezi Agosti, 2019 kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi mwezi Agosti, 2020. Mkutano huo unafanyika kwa mara ya kwanza visiwani Zaznibar huku ukiwa na fursa kubwa kwa wananchi kwani utasaidia kukuza biashara na utalii na kujitangaza kimataifa.
Kauli mbiu ya Mkutano huu:Ushiriki wa kisekta kwenye kupunguza madhara ya maafa ni njia bora ya kuimraisha ustamilivu katika ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini wa Afrika (SADC).”
Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya Menejimenti ya Maafa imeanzishwa kwa lengo la kulishauri Baraza la Mawaziri wa nchi za SADC kuhusu masuala ya upunguzaji wa madhara ya maafa kikanda huku lengo mahususi likiwa ni kuwa na jukwaa la kubadilishana taarifa na uzoefu wa kiutendaji.