Home Mchanganyiko DK. AGNES KIJAZI ATANGAZA UTABIRI WA MWELEKEO WA MSIMU WA MVUA ZA...

DK. AGNES KIJAZI ATANGAZA UTABIRI WA MWELEKEO WA MSIMU WA MVUA ZA MASIKA KWA KIPINDI CHA MWEZI MACHI HADI MEI 2020

0

 

Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania TMA Dk. Agnes Kijazi akizungumza wakati akitangaza taarifa ya  utabiri wa hali ya MWELEKEO WA MSIMU WA MVUA ZA MASIKA KWA KIPINDI CHA MWEZI MACHI HADI MEI 2020 katikati ni Dk. Hamza Kabelwa MKurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA na kushoto ni Rose Senyagwa Mtaalam wa Hali ya Hewa.

 Rose Senyagwa Mtaalam wa hali ya hewa kutoka TMA wakati akitoa taarifa ya utabiri  wa hali ya hewa msimu uliopita kabla ya kumkaribisha Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk. Agnes Kijazi )katikati ni Dk. Hamza Kabelwa Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA.

Baadhi ya vielelezo vya utabiri wa mvua hizo za masika.

………………………………………………………

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini TMA Dkt. Agnes Kijazi leo ametangaza taarifa ya utabiri wa hali ya hewa mwenendo wa mvua za masika katika kipindi cha Machi – Mei, 2020 wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya taasisi hiyo Jengo la Ubungo Plaza jijini Dar es salaam.

Dk. Kijazi ametoa taarifa inayotoa uchambuzi wa mwenendo wa mvua za masika katika kipindi cha Machi – Mei, 2020 ikiwa ni pamoja na mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu.

Ametoa ushauri kwa wadau wa sekta mbalimbali kama vile Kilimo
na Usalama wa Chakula, Mifugo na Wanyamapori, Maliasili na Utalii, Nishati na Maji, Mamlaka za Miji, Afya pamoja na Menejimenti za Maafa ili kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua za masika ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea kutokana na mvua hizo.

Taarifa hiyo imeelezea utabiri huo imesema kuwa mvua za Masika kwa kipindi cha Machi hadi Mei, 2020 zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya mkoa wa Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba, maeneo mengi ya mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, mashariki mwa mkoa wa Geita pamoja na mikoa ya
Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara.

Maeneo ya mkoa wa Kagera, magharibi mwa mkoa wa Geita, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Pwani (ikijumuisha kisiwa cha Mafia) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa
Morogoro yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.

Taarifa hiyo imeelezea kwamba Mvua za nje ya msimu zinazoendelea kunyesha katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, hususan yaliyopo katika pwani ya kaskazini zinatarajiwa kuendelea na kuungana na msimu wa mvua wa Masika 2020.

Athari zinazotarajiwa ni pamoja na Mvua za kutosha katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, zinatarajiwa kunufaisha uzalishaji wa mazao mbalimbali yakiwemo yale yanayostahimili unyevunyevu mwingi ardhini kama vile mpunga. Aidha, uwepo wa malisho na maji ya kutosha kwa ajili ya mifugo na wanyamapori vinatarajiwa ambapo milipuko ya magonjwa na wadudu waharibifu vinaweza kujitokeza kutokana na hali ya unyevunyevu na kutuama kwa maji.

Taarifa hiyo imetahadharisha kuwa Uchimbaji wa madini ufanyike kwa kuzingatia utabiri uliotolewa kwani ongezeko la maji katika udongo linaweza kusababisha maporomoko ya ardhi hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Imeeleza kuwa vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, hivyo jamii inashauriwa kuchukua hatua stahiki
kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Taarifa imeongeza kuwa Msimu wa mvua za Masika ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini-mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia Tanga na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro ikiwa ni pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

Kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na jinsi inavyotarajiwa kuwa kwa kipindi chote cha msimu (kama ilivyoelezwa katika kipengele cha III cha taarifa hii), kwa ujumla
mvua za wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

Hata hivyo, maeneo mengi ya nyanda za juu kaskazini mashariki,
mashariki na kusini mwa Ziwa Viktoria, mkoa wa Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani. Aidha, maeneo ya  magharibi mwa Ziwa Viktoria na maeneo mengine ya pwani ya kaskazini (Mikoa ya Dar es salaam, Pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro) yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.

Taarifa hiyo ya hali ya hewa inaendelea kueleza kuwa Kanda ya Ziwa Viktoria: (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, na Mara): Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya mashariki mwa mkoa wa Geita, mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara. Aidha, mvua za wastani hadi
chini ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kagera, magharibi mwa mkoa wa Geita na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma (Wilaya za Kakonko na Kibondo). Mvua hizi zinatarajiwa kuanza katika wiki ya pili ya mwezi Machi, 2020 na kuisha kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Mei, 2020.

Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba): Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya mkoa wa Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba. Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani (ikijumuisha kisiwa cha Mafia) pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani. Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza kati
ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Machi 2020 na zinatarajiwa kuisha katika wiki ya tatu ya mwezi Mei, 2020. Aidha, mvua zinazoendelea katika maeneo haya zinatarajiwa kuungana
na mvua za msimu wa Masika, 2020.

 Taarifa hiyo imemalizia kuwa Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro): Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi.

Mvua hizo zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Machi, 2020 na kuisha kati ya wiki ya pili na tatu ya mwezi Mei, 2020.