Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kushoto) akibadilishana mawazo na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa ajili ya kuanza ziara ya kukagua shughuli za madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini tarehe 12 Februari, 2020.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Wilfred Machumu (kushoto) akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) kwenye machimbo ya kokoto ya Nyakamtwe mkoani Njombe.
Shughuli za upondaji wa kokoto zikiendelea katika eneo la Matarawe mkoani Njombe.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) akitoa maelekezo kwa Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Wilfred Machumu (katikati) katika eneo la Matarawe mkoani Njombe.
Soko Kuu la Dhahabu na Vito Njombe
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akikagua madini ya mchanga kwenye machimbo ya Mtwango mkoani Njombe
…………………………………………………………………………………………………
Na Greyson Mwase, Njombe
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini imeweka mikakati ya kuhakikisha madini yanawanufaisha watanzania pamoja na kukuza uchumi wa nchi.
Profesa Kikula ametoa kauli hiyo katika nyakati tofauti kwenye ziara yake aliyoifanya leo tarehe 12 Februari, 2020 mkoani Njombe yenye lengo la kufuatilia maelekezo aliyoyatoa katika ziara yake aliyoifanya awali nchini kati ya tarehe 29 Oktoba, 2019 na tarehe 03 Novemba, 2019, kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wachimbaji wa madini.
Katika ziara yake kwenye machimbo ya madini, Profesa Kikula aliambatana na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Wilfred Machumu, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Njombe anayeshughulikia Uchumi na Uzalishaji, Gumbo Mvanda pamoja na wataalam kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, na Tume ya Madini Makao Makuu.
Profesa Kikula alifafanua kuwa ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika na rasilimali za madini, Serikali ilifanya maboresho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 ili kuhakikisha wananchi wanakuwa sehemu ya uchumi wa madini kwa kujipatia kipato na kulipa kodi mbalimbali Serikalini.
Katika hatua nyingine, Profesa Kikula aliwataka wananchi kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo kwenye Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma kwenye kampuni zinazojihusisha na utafiti na uchimbaji wa madini na kuunda vikundi vidogo ili kupewa leseni za madini na kuanza kuchimba mara moja.
Akielezea mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini, Profesa Kikula alifafanua kuwa ni pamoja na kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli ambapo katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali ilikusanya jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 346 ikiwa imevuka lengo lililopangwa la kukusanya shilingi bilioni 310.
Alieleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja uanzishwaji wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa pamoja na Maafisa Migodi Wakazi kwenye maeneo yenye migodi mikubwa ya madini, uanzishwaji wa masoko ya madini pamoja na vituo vya ununuzi wa madini.
Aliendelea kusema kuwa ili kuhakikisha huduma katika shughuli za utafiti, uchimbaji na biashara ya madini zinaimarika nchini, Serikali imeongeza wataalam kwenye Ofisi za Madini, vitendea kazi ikiwa ni pamoja na magari na mashine za kupima madini kwenye masoko ya madini yaliyoanzishwa.
Aidha, Profesa Kikula aliwataka wamiliki wa leseni za madini kuhakikisha wanaandaa na kutekeleza mipango ya ufungaji wa migodi ili kuepusha athari za uharibifu wa mazingira zinazoweza kujitokeza mara baada ya kumalizika kwa shughuli za uchimbaji wa madini.
Vilevile aliwataka wachimbaji wa madini kuendesha shughuli zao kwa kufuata Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.