Home Mchanganyiko MENEJIMENTI YA NCAA YAPIGA KAMBI KRETA YA NGORONGORO KUSIMAMIA UBORESHAJI WA MIUNDOMBINU

MENEJIMENTI YA NCAA YAPIGA KAMBI KRETA YA NGORONGORO KUSIMAMIA UBORESHAJI WA MIUNDOMBINU

0

Kamishna wa Uhifadhi wa mamkaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Freddy Manongi (katikati) akijadiliana jambo na Meneja Manunuzi wa NCAA Bw. John Laizer (kushoto) kuhusu uboreshaji wa barabara katika bonde la Ngorongoro la Kreta.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Prof. Adolf Mkenda kushoto akiwa na Naibu Kamishna wa NCAA Bw. Asangye Bangu alipotembelea baadhi ya vipande vya barabara vilivyoathirika na mvua hivi karibuni.

……………………………………………………………………………………………………

 

Na Kassim Nyaki-NCAA

Menejimenti ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)  ukiongozwa na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka hiyo Dkt Freddy Manongi imeweka kambi katika kreta ya Ngorongoro ili kuongeza nguvu ya usimamizi wa ukarabati wa vipande vya barabara vilivyoathirika katika bonde la kreta ya ngorongoro kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Dkt Manongi akiwa ameambatana na baadhi ya wajumbe wa menejimenti ya NCAA amebainisha kuwa mvua zilizoanza kunyesha tangu mwezi septemba mwaka jana 2019 zimeleta athari kubwa katika bonde la kreta ya Ngorongoro na sasa baada ya kupungua kwa takribani siku mbili wameamua kuhamishia ofisi ndani ya Kreta hiyo kuendelea na usimamizi wa karibu katika kuimarisha maeneo machache yaliyoathirika kwa uharaka.

Kamishna Manongi ameongeza kuwa tayari wameshafanya tathmini ya sehemu zilizoathirika zaidi na sasa wanafanya juhudi ya kuongeza vifaa pamoja na nguvu kazi ya wataalam wa ujenzi ili kuendana na kasi ya kuimarisha miundombinu iliyoharibika katika muda mfupi ujao.

“Tumeshafanya tathmini ya maeneo yote yaliyoathirika na sasa juhudi zinazoendelea ni kuongeza vitendea kazi hasa magari na nguvu kazi ya wataalam ili tuweze kuimarisha miundombinu hii kwa haraka na kuepusha adha kwa wageni wetu.

Katokana na changamoto ya kukwama kwa baadhi ya magari ndani ya kreta, uongozi wa Mamlaka hiyo umeweka magari na askari kwa ajili ya kutoa msaada kwa wageni na madereva wa gari za utalii inapotokea changamoto yoyote hasa kukwama au kuharibika kwa magari katika maeneo yenye changamoto ya miundombinu.

“Wakati tukiendelea na shughuli za ukarabati wa barabara za kreta, tunaomba wadau wetu wawasiliane nasi kwa namba 0623453870 na 0787153870 kama utaharibikiwa na gari ama kukwama ili NCAA tutoe msaada, tumeweka magari ya kusaidia usumbufu wowote unaoletwa na changamoto za mvua ili tuweze kuuondoa, poleni sana tuko kazini” aliongeza Dkt Manongi.