…………………………………………………………………………………………..
NA MWAMVUA MWINYI,RUFIJI
KAYA zaidi ya 500 zimekumbwa na maafa ya mvua,huku hekari zaidi ya 20,000 zilizolimwa mazao mbalimbali ,jimbo la Rufiji,mkoani Pwani, zimesombwa na maji ya mvua ambayo yanatiririka kutoka Nyanda za Juu Kusini ikiwemo mikoa ya Morogoro na Iringa.
Aidha inajengwa hofu kubwa ,kwa baadhi ya watu wakihofia athari kubwa kuja kutokea ya baa la njaa kutokana na maji kuongezeka na kusomba mazao huku maji mengine yakiwa yameshafunguliwa Mtera .
Akizungumzia athari hiyo ,mbunge wa jimbo la Rufiji ,Mohammed Mchengerwa alisema ,kata karibia zote za jimbo hilo zimeguswa na maafa hayo,ikiwemo Muhoro,Chumbi ,Umwe na Ikwiriri.
Alisema, hadi sasa hekari 5,000 za mazao katika kata ya Muhoro zimesombwa na maji na kata ya Chumbi hekari zaidi ya 8,000.
Mchengerwa alieleza, wananchi zaidi ya 20,000 wanaoishi Muhoro wanapata shida kwa sasa kwa kuwa wanategemea kupata huduma za kijamii ikiwemo afya na elimu kwa kuvuka ng’ambo ya pili ambapo ndipo kuna mahitaji.
Alieleza,wanahamisha mifugo na familia ambazo nyumba zao zimejaa maji na nyingine kusombwa na mvua kuzipeleka katika maeneo yaliyo salama.
“Kimsingi mvua kwa hapa Rufiji si kubwa sana ,ila hili tatizo linasababishwa na maji kutoka Nyanda za Juu Kusini mikoa ya Iringa,Morogoro,yanatiririka kwenye mabonde na mabwawa,hofu kubwa inakuja kwamba Mtera nayo imeshafunguliwa siku tatu ,tano zijazo hali itakuwa mbaya zaidi ya hii”:
“Nimelazimika kuleta fedha za mafuta ya boti ili kuvusha watu ,na wanafunzi ili waweze kwenda shule, japo pia hii sio njia salama kwao”
“Hizi boti ni za watu binafsi hivyo pia nimeamua kulipia fedha wazee wasiojiweza, wajawazito,wagonjwa,wasio na uwezo na wanafunzi ili waweze kuvushwa kutokana na kushindwa kuwa na fedha hizo”alifafanua Mchengerwa.
Mchengerwa alibainisha, kwasasa anashirikiana na Halmashuri kuangalia uwezekano wa kupata boti ya kuhudumia wanafunzi peke yao ili wasikose kwenda kusoma.
Hata hivyo ,mbunge huyo alieleza ameshachukua hatua ya kuzungumza na waziri pamoja na mkurugenzi wa maafa juu ya maafa hayo na aliiomba serikali kufika katika maeneo hayo kujionea athari iliyopo .
Mkuu wa wilaya ya Rufiji ,Juma Njwayo alisema ,serikali na mamlaka husika imeona maafa hayo na inashughulikia suala hilo.
Alitoa pole kwa wote waliokumbwa na maafa hayo na kusema serikali ipo pamoja nao .
3 Attachments