Daktari Bingwa Ubongo, Uti wa Mgongo Mishipa ya Fahamu Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Mohamed Mnacho akizungumza na wakazi wa Manzase Bakhera kuhusu ugonjwa wa kifafa.
Wakazi wa Manzese wakifuatilia elimu kuhusu kifafa iliyokuwa inatolewa na Madaktari Bingwa Ubongo, Uti wa Mgongo Mishipa ya Fahamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH).
Daktari Bingwa Ubongo, Uti wa Mgongo Mishipa ya Fahamu Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Kigocha Okeng’o akizungumza na wakazi wa Manzase Bakhera kuhusu ugonjwa wa kifafa.
Wasanii wa kundi cha Sanaa za Maonyesho cha Senene Culture group wakionyesha igizo la namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa mgonjwa wa kifafa.
Mmoja wa wakazi wa Manzese (Kushoto), akiuliza swali kuhusu ugonjwa wa kifafa, Kulia ni Daktari Bingwa Ubongo, Uti wa Mgongo Mishipa ya Fahamu Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt.Patience Njenje.
………………………………………………………………………………………….
Madaktari Bingwa Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH) wametoa elimu kwa umma kuhusu ugonjwa wa kifafa katika eneo la Manzese Bakhera katika kuadhimisha siku ya kifafa duniani inayofanyika kila jumatatu ya pili ya mwezi Februari duniani kote lengo ikiwa ni kuwaelimisha wananchi kuhusu ugonjwa huo.
Akizungumza wananchi wa Manzese Dkt. Petience Njenje amesema kuwa kifafa ni ugonjwa unaotokana na hitilafu au jeraha kwenye ubongo linalosababisha mgonjwa kuanguka, kukakamaa kuzimia au kutokuzimia na wakati mwingine kutoa povu mdomoni.
Idadi ya wagonjwa wa kifafa Tanzania inakadiriwa kuwa milioni moja.Wanaoishi na tatizo la kifafa wako katika hatari ya kifo mara sita zaidi ukilinganisha na jamii yote kwa ujumla.Wagonjwa wengi wa kifafa ni vijana, wakiwa na umri wa wastani wa miaka 15.
“Zaidi ya 75% ya wagonjwa wa kifafa Tanzania huenda kutafuta tiba kwa waganga wa kienyeji na viongozi wa dini wakiamini kuwa mgonjwa amevamiwa na mapepo mabaya au mashetani.60% ya wagonjwa wanaofika kupata tiba hospitalini hufika mwaka mmoja baada ya kupata tatizo. Ni kati ya 5-10% ya wagonjwa wa kifafa Tanzania ndio hupatiwa matibabu hospitalini hivyo wengi wanaoishi na kifafa Tanzania wana kifafa ambacho ni cha kiwango cha juu sana” amesema Dkt. Njenje
Naye Dkt. Kigocha Okeng’o amesema kuwa kifafa husababishwa na homa kali kipindi cha utoto ,ajali zinazoleta majeraha kwenye ubongo, matatizo ya kipindi cha ujauzito na wakati wa kujifungua pamoja na minyoo sugu.
“Tunatoa wito kwa wananchi kujikinga na visababishi vinavyozuilika kama kumjali mama mjamzito kipindi cha ujauzito kwa kumshauri kuhudhuria kliniki pamoja na kumpatia vipimo mara kwa mara, kufanya uchunguzi na watoto kupata matibabu ya wanapopata homa; matumizi ya choo, kunawa mikono na kula nyama ya nguruwe iliyoiva vizuri” amesema Dkt. Kigocha.
Kuhusu Tiba ya kifafa Dkt. Edward Kija amesema kuwa kifafa kinatibika endapo mgonjwa atafikishwa hospitalini mapema na atatumia dawa kwa kipindi kirefu bila kuacha.
Naye Mkazi wa Manzese Bw. Julius Masha amewashukuru madaktari kwa elimu walioitoa kuhusu kifafa kwa kuwa imewasaidia kujua dhana nzima ya kifafa na namna sahihi ya kuishi na mgonjwa mwenye tatizo hilo.