NA EMMANUEL MBATILO-0673956262
Mradi wa Ujenzi wa Reli ya kisasa wa Standard Gauge Railway (SGR) ni miongoni mwa miradi ambayo Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt.John Pombe Magufuli , Rais amekuwa akihakikisha nchi ndani ya uongozi wake kufufua viwanda pamoja na kuboresha miundombinu ambayo itasaidia kufikia nchi ya viwanda kama kauli yake ambayo inasema NCHI YA VIWANDA hivyo usafiri wa reli ni miongoni mwa usafiri ambao utasaidia wafanyabiashara kusafirisha mizigo yao kwa haraka na wepesi.
Lakini ili kuweza kutimiza malengo hayo ni lazima wananchi kwa ujumla tuunge mkono juhudi hizi hasa kwa kulipa kodi maana miradi yote hiyo inategemewa na kodi za wananchi wenyewe.
Ndo maana Mhe.Rais amekuwa akipambana kuhakikisha anawashughulikia wakwepa kodi wote ambao wamekuwa ni kikwazo katika kufikia malengo ya nchi yetu.
Wananchi kwa ujumla tunatakiwa kuwa walinzi wa miundombinu inayojengwa na serikali kwa sababu kumekuwa na baadhi ya watu ambao si wema wamekuwa wakiharibu miundombinu inayojengwa.
Shirika la reli Tanzania (TRC) hivi karibuni lilibaini kuwepo kwa baadhi ya watu ambao wanaharibu na kuiba baadhi ya vifaa vya ujenzi wa reli, hii ina maana tukiendelea hivyo tutakuwa tunarudisha nyuma maendeleo na kuchelewesha kufikia malengo ambayo tumejiwekea kama nchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya usalama katika reli hivi karibuni, Kaimu mkurugenzi wa TRC, Bw. FOCUS SAHANI alisema kuwa ili kuimarisha usalama katika reli inapaswa kila mwananchi na wadau binafsi kuwa walinzi na kutoa taarifa za vitendo vya hujuma hizo polisi ili kuhakikisha wahujumu hao wanachukuliwa hatu za kisheria na kupata adhabu wanayostahili wanapopatikana na hatia ya kutenda makosa hayo.
“Mara kadhaa kumekuwa na matukio ya baadhi wananchi wasio raia wema wanajaribu kuiba ama kufanya hujuma kwa kutega vyuma relini. Serikali inatambua vitendo vinayofanyika katika maeneo hayo wanakojaribu kuhujumu ama kutega treni ,wapo raia wema wanaotoa taarifa”. Amesema Bw.Sahani.
Hata hivyo kwa upande wake Kaimu kamishina wa jeshi la polisi kikosi cha usalama wa reli Stanley Kulyamo alisema kikosi hicho tayari kinawashkilia watu kadhaa kutokana na makosa ya uharibifu wa miundombinu ya reli na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabiri.
Ijumaa, Februari 7, 2020 , akisoma hotuba yake ya kuahirisha mkutano wa 18 wa Bunge la 11 bungeni jijini Dodoma Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa alisema kuwa ujenzi ulipofikia wa mradi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge ni hatua kubwa hata hivyo mafanikio hayo yametokana na kuimarika kwa mapato.
Alisema hatua hiyo ni miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba, 2019.
Alisema kazi za ujenzi kwa sehemu ya Morogoro – Makutupora (kilometa 422) zinaendelea vizuri na Serikali imerejesha huduma ya reli ya abiria na mizigo ya Kaskazini (Dar es Salaam – Moshi).
Mpaka sasa mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa Standard Gauge Railway (SGR) umefikia asilimia 72 kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shirika la Reli hapa nchini Bw.Masanja Kadogosa, hii ni hatua kubwa kwani mpaka sasa malengo ambayo nchi inahitaji kufikia inaleta matumaini.
Kadogosa alieleza kuwa TRC imefanikiwa kuongeza idadi ya mizigo ambapo zaidi ya tani 1,456,537 zimeweza kusafirishwa katika reli ya kati (Dar es Salaam, Mwanza na Kigoma) na kwa upande wa abiria treni za mikoani wameongezeka kutoka 411,172 mwaka 2014/15 hadi 578,439 mwaka 2018/19.
Sambamba na hilo, TRC imeweza kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 17.4 mwaka 2014/15 hadi bilioni 30 mwaka 2018/19 kwa treni za mizigo, kutoka bilioni 8.3 hadi bilioni 10.7 kwa treni za abiria wa mikoani na kutoka milioni 316.6 hadi bilioni 1.96 kwa treni za mjini.
Aidha TRC inajivunia mageuzi makubwa yanayofanywa na Serikali katika sekta ya reli kwa kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) wenye gharama ya shilingi trilioni 7.5
Kuna baadhi ya wadau mbalimbali nchini na nje ya nchi wamekuwa mstari wa mbele kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha nchi yetu inatimiza lengo la kufikisha uchumi wa kati hasa katika kuboresha viwanda ambavyo vitasaidia kufikia uchumi huo.
Rais na Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Dkt. Admassu Tadesse wakatialipotembelea mradi huo mwaka jana aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR) kwa kutumia fedha zake za ndani na kuahidi kuwa Benki yake itafanya kila linalowezekana kuhakikisha inatafuta fedha za kujenga reli hiyo.
Dkt. Tadesse alitoa kauli hiyo alipotembelea sehemu ya ujenzi wa miundombinu ya reli hiyo, kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro na kujionea kazi kubwa iliyofanyika ambapo amesema mradi huo hautainufaisha Tanzania peke yake bali pia nchi za ukanda wa Afrika hususan ambazo hazipakani na Bahari.
Kiongozi huyo wa juu wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Dkt. Tadesse, alieleza kuwa mwaka huu Benki yake imeipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani bilioni moja sawa na takribani sh. za Tanzania trilioni 2.3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi yake mikubwa ya maendeleo.
Alisema Tanzania imenufaika pia na kiasi kingine cha zaidi ya dola za Marekani bilioni moja zilizotolewa na Benki yake miaka ya nyuma na ameelezea kufurahishwa kwake na namna nchi inavyokua kwa kasi kiuchumi na kwamba inakopesheka.
Hata hivyo kiongozi huyo aliahidi kuwa kwa kuwa fedha zinazohitajika kukamilisha ujenzi wa mradi huo wa reli ya kisasa ni nyingi, Benki yake itazishawishi taasisi nyingine za fedha ndani na nje ya Bara la Afrika kuchangia ujenzi huo ili mradi ukamilike kwa wakati ili kuchochea masuala ya Bashara na kuboresha shughuli za usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo.
Hii ni hatua kubwa lazima tujipongeze kwa hatua tuliofika hasa kwa serikali hii ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa Kauli Mbio yake ya Tanzania ya Viwanda.