Home Makala   James Bokella-TBL ni tanuru la kupika wataalamu wa viwanda, mauzo na...

  James Bokella-TBL ni tanuru la kupika wataalamu wa viwanda, mauzo na masoko

0

James Bokella akiwa katika majukumu yake ya kazi

********************************

“MASOKO, ni moja ya taaluma nyeti inayofanikisha  kukuza biashara  na itakayosaidia kufanikisha azma ya serikali ya awamu ya tano kujenga uchumi wa kati unaoongozwa na sekta ya viwanda, kwa kuwa bidhaa zikizalishwa lazima ziingie katika masoko,” anasema James Bokella, mtaalamu wa Mauzo nchini ambaye ni Mkurugenzi wa Biashara wa Kanda ya Kaskazini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

Bokella, anasema kuwa bila kuwepo na wataalamu wa fani ya mauzo na masoko wenye weledi mkubwa bidhaa zitakazozalishwa viwandani, zitashindwa kuingia katika masoko  na kuhimili ushindani mkubwa wa bidhaa uliopo katika masoko ya ndani na  kimataifa, zikikosa masoko viwanda haviwezi kujiendesha kwa faida na ukuaji wa  sekta hiyo utakuwa mdogo.

Katika mahojiano hivi karibuni,Bokella,alisema baada ya kuhitimu masomo yake ya shahada ya kwanza alipata ajira Serikalini na baadaye alijiunga  na Kampuni  ya Kibo Breweries Ltd na kisha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ,tangia  mwaka 2002 katika kitengo cha Mauzo na Masoko. Ameweza kushika nafasi mbalimbali kuanzia Umeneja  Mauzo wa mikoa, Meneja Mauzo wa Taifa (National Sales Manager), na mpaka sasa ni Mkurugenzi wa Biashara wa Kanda.

Anasema anajivunia kuwa mwajiriwa wa kampuni kubwa kama TBL ambayo ni mlipa kodi mkubwa nchini, kwa kuwa imemwezesha kupata fursa ya kijifunza mambo mengi  kuhusiana na taaluma ya Mauzo, Masoko na Usambazaji kupitia kozi za ndani na nje ikiwemo kufanya kazi nje ya Tanzania nchini Afrika ya Kusini katika viwanda vya iliyokuwa kampuni mama ya TBL – SABMiller Plc. Licha ya kuwa ni kampuni yenye uhodhi mkubwa wa soko hapa nchini pia kampuni imewekeza katika mifumo ya kimataifa ya usambazaji bidhaa zake ambayo kuitumia kunahitaji weledi mkubwa.

“Najisikia furaha kuwa mmojawapo wa wafanyakazi waandamizi wa Kitanzania wa TBL, nimepata mafanikio mengi, nafurahi kuwa mmoja wa Watanzania tunaoendelea kutoa mchango mkubwa katika sekta ya viwanda nchini ambayo ndiyo azma kuu ya Serikali ya awamu ya tano (Uchumi wa Viwanda),pia ajira yangu inaniwezesha kuihudumia vizuri familia yangu, “.anasema Bokella

Kuhusiana na elimu yake Bokella alisema anayo Shahada ya Uzamili (Masters) ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Aberdeen (UK) pia amehudhuria kozi mbalimbali za mauzo, masoko na usambazaji ndani na nje ya nchi.

Mbali na shahada hiyo anasema akiwa mwajiriwa wa kampuni ya TBL, ameweza kupata mafunzo mengi kuhusiana na mifumo bora ya mauzo, masoko na usambazaji ambayo inamwezesha kufanya  kazi yake kwa uhakika zaidi. ”Kazi yangu naifahamu vizuri na kuimudu na najivunia kuwa miongoni mwa wataalamu wa fani  hii nchini”. Alisema kwa kujiamini.

Alisema kutokana na uchapakazi wake katika kipindi chake cha ajira ameweza kutunukiwa tuzo mbalimbali na kampuni ambazo baadhi yake amezitaja kuwa ni Masters Certificate 2012 (SABMiller Africa), MS&MD Gold Award 2014 (SABMiller Africa, ABI Partners Award 2017 (ABInBev-Global)

Pia alisema kuwa anaweza kufanya kazi zake vizuri kutokana na ushirikiano mzuri anaopata kutoka kwa wafanyakazi wenzake “TBL, ni tanuru la kupika wataalamu na imeajiri watu wenye uwezo mkubwa katika fani zao hivyo nafanya kazi na wataalamu ambao wana upeo mkubwa na wanaoelewa nini wanachokifanya bila kuhitaji usimamizi mkubwa.

Kuhusu changamoto anazokumbana nazo katika kazi yake, alisema ni za kawaida na kutokana na elimu yake na uzoefu wa kazi alionao anaweza kuzitatua kwa urahisi na maisha kuendela kama kawaida.

Malengo yake ya baadaye baada ya kustaafu kazi ni kujiajiri kwa kufanya kazi za ushauri wa kitaalamu wa fani yake ya Uchumi hususan Mauzo na Masoko ambayo anaamini kuwa inazidi kukua na kuhitaji wataalamu tofauti na ilivyokuwa  miaka ya nyuma.

Gwiji huyu ambaye amefanya kazi ya mauzo,masoko na usambazaji kwenye sekta ya bia kwa zaidi ya miaka 20 ametoa ushauri kwa vijana wa Kitanzania ambao wako vyuoni wasome kwa bidii sambamba na kuwa wabunifu ili waje na mifumo itakayo rahisisha kazi walizosomea watakapoanza kuzifanya kwa vitendo badala ya kukariri masomo ya nadharia yanayopatikana kwenye vitabu.

Alimalizia kwa kuwaasa vijana kuacha tamaa ya maisha na kuwa wavumilivu, kutulia na kuwa tayari kujifunza. “Vijana wengi wa siku hizi wanakuwa sio wavumilivu na wanapanga malengo makubwa ambayo inakuwa vigumu kuyafikia kwa muda mafupi matokeo yake baadhi wanajikuta wamejiingiza kwenye vitendo potofu na kusababisha wasiaminike na  waajiri wao”.

Bokella, alisema baada ya majukumu yake ya kazi anapendelea kuwa karibu na familia yake (mkewe Yasinta na watoto wake Ken na Nik) sambamba na kushiriki katika shughuli nyingine za kijamii.Vilevile ni mpenzi wa mpira wa miguu,muziki,kusoma majarida na kuangalia habari hususani za kimataifa.Vinywaji anavyopendelea kupata baada ya saa za kazi ni bia aina ya Castle Lite, Ndovu Special Malt na Budweiser.