Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akipeana mkono na Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya, baada ya Mkutano kati yao uliofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akielezea umuhimu wa kuboreshwa kwa Idara ya Forodha kwa lengo la kuongeza urahisi wa ufanyaji wa biashara, wakati wa Mkutano na Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya (hayupo pichani), kulia ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya (kulia), akieleza nia ya Shirika lake kusaidia zana za Kisasa katika Idara ya Forodha nchini, wakati wa Mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani), jijini Dodoma, kushoto ni Meneja Uwezeshaji wa Biashara na Ujenzi wa Miundombinu Mipakani kutoka WCO, Bw. Kosaka Yoshihiro.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) (kushoto), akimuomba Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya (katikati) kusaidia katika kuondoa vikwazo vya wafanyabiashara wa Tanzania kuuza bidhaa zao katika masoko ya Kimataifa, kulia ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede, katika Ofisi za Wizara hiyo eneo la Mtumba, jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati) na Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya (wa pili kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede (wa pili kulia) na viongozi wengine, baada ya Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) (wa pili kushoto) na Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya (kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede (wa pili kulia) na viongozi wengine, baada ya mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mtumba jijini Dodoma.
(Picha na Veronika Kazimoto na Peter Haule)
*******************************
Na. Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali imekubaliana na Shirika la Forodha Duniani (WCO) kuisaidia nchi zana zenye teknolojia za kisasa zinazoweza kung’amua watu wanaofanya biashara za magendo na kuifanya Forodha kuongeza ufanisi wa ufanyaji biashara na ukusanyaji wa mapato.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alipokutana nan a kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya, jijini Dodoma.
Dkt. Mpango alisema kuwa Shirika la WCO limekubali kutoa Boti, mashine za kupiga picha ndani ya Kontena na vifaa vingine vyenye teknolojia za kisasa vinavyoweza kung’amua watu wanaofanya biashara za magendo, hivyo kuifanya Serikali kuwa na uwezo zaidi wa kudhibiti shughuli hizo haramu.
“Ujio wa Katibu Mkuu wa WCO, katika nchi za Afrika hususani Tanzania na Kenya umelenga kuziwezesha nchi hizo kuzitumia fursa zilizopo katika Shirika hilo na kushirikiana na Idara ya Forodha hapa nchini kurahisisha biashara na ukusanyaji wa mapato jambo ambalo pia ni agenda ya Serikali ya Tanzania”, alieleza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango alisema kuwa, Forodha kwa maana ya Bandari na Vituo vya Forodha vilivyopo katika mipaka ni eneo muhimu katika kukuza biashara katika nchi na Ukanda wa Kusini mwa Afrika, ikizingatiwa kuwa Tanzania ni mlango wa kupitisha mizigo kwenda nchi za Zambia, Zimbabwe, Rwanda, Burundi, Malawi, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nyingine, hivyo kuwepo kwa Teknolojia hiyo kutakuwa nguzo muhimu ya kuifanya Forodha kuwa ya Kisasa na inayorahisisha biashara.
Alisema kuwa wamekubaliana kutoa fursa kwa vijana wa Forodha kupata uzoefu wa Forodha nyingine zinavyoendeshwa kwa ufanisi na pia kutoa mafunzo kwa wakufunzi ambao si tu watatoa mafunzo nchini lakini pia nje ya nchi.
Wakati huo huo, Dkt. Mpango amewaonya wafanyabiashara za magendo nchini kuachana na biashara hiyo kwa kuwa watapoteza mitaji baada ya Serikali kujipanga kwa teknolojia mpya ya kuwadhibiti kwa kuwa biashara hizo ni hatari kwa uchumi wa Taifa na pia Afya za wananchi.
“Wito wangu ni kwamba watanzania wote na wengine walio nje ya nchi wanaoshiriki katika biashara za magendo waache vitendo hivyo na wafuate taratibu za Forodha kinyume na hapo watapoteza mitaji yao kwa kuwa tutawakamata’’, alieleza Dkt. Mpango
Waziri Mpango amemuagiza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede, kuhakikisha Ushirikiano na WCO unaimarika kwa kuwa Shirika hilo lina manufaa kwa Maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Dkt. Kunio Mikuriya, alisema kuwa katika kuifanya Forodha iwe na ufanisi lazima kuwe na dhamira njema ya kisiasa, Ushirikiano na wafanyabiashara,wakala na Forodha nyingine nje ya nchi na pia kuwekeza kwenye rasilimali watu, jambo ambalo amehakikishiwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mpango kwamba lipo.
Dkt. Mikuriya ameahidi kuwa Shirika lake litafanya kazi kwa karibu na Tanzania katika mambo yote ambayo wamekubaliana ili kuleta tija katika Sekta hiyo ya Forodha ndani na nje ya Tanzania.
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa, ameliomba Shirika la WCO kuondoa changamoto zinazoweza kuwakwamisha wafanyabiashara wa Tanzania kuuza bidhaa katika masoko ya Kimataifa na pia waweze kuzitumia fursa za kibiashara katika masoko hayo.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede, alisema kuwa wamekubaliana na Shirika la WCO, kujenga Maabara ambayo itasaidia kutambua na kupima bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi ili kujiridhisha kama zimezingatia utaratibu, lengo likiwa ni kurahisisha uthaminishaji wa mizigo na uondoshaji wa mizigo bandarini kwa wakati.
“Maabara hiyo itakayojengwa katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Jijini Dar es Salaam, itakua miongoni mwa maabara chache Afrika ambayo itakuwa ya mfano katika kusimamia eneo hilo la Forodha”, alieleza Dkt. Mhede.
Alisema kuwa wamekubaliana pia kuweka miundombinu itakayochunguza mizigo inayopita katika Ukanda wa Kusini (Mtwara Corridor), ikizingatiwa kuwa barabara ya Ukanda huo imesajiliwa kwa lengo la kuhakikisha Wajasiliamali na wenye viwanda wanaitumia kwa tija.