Home Mchanganyiko TANZANIA YAISHAURI ETHIOPIA KUTAFUTA KIINI CHA TATIZO LA WAHAMIAJI HARAMU

TANZANIA YAISHAURI ETHIOPIA KUTAFUTA KIINI CHA TATIZO LA WAHAMIAJI HARAMU

0

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia Dkt Workneh Gebeyehu walipokutana kwa ajili ya mazungumzo Mjini Addis Ababa,Ethiopia Kando ya Mkutano wa 33 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia Dkt Workneh Gebeyehu. Mazungumzo hayo yamefanyika Mjini Addis Ababa,Ethiopia Kando ya Mkutano wa 33 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika. kushoto aliyevaa kilemba ni Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia Mhe Naimi Azizi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia Dkt Workneh Gebeyehu (Katikati) akiwa na ujumbe wake katika mazungumzo baina yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb).Mazungumzo hayo yamefanyika Mjini Addis Ababa,Ethiopia Kando ya Mkutano wa 33 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika.
********************************

Tanzania imeishauri Nchi ya Ethiopia kuchukua hatua ya kuchunguza kiini cha raia wake kuondoka nchini humo kinyume na utaratibu na kwa njia zisizo halali jambo linalosababisha  mrundikano wa wafungwa ambao wanakamatwa katika nchi wanazopita kama wahamiaji haramu ikiwemo Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ametoa ushauri huo Addis Ababa Ethiopia anakohudhuria mkutano wa 33 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika na kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia kando ya mkutano huo Dkt. Workneh Gebeyehu na ili kuchukua hatua za kudhibiti idadi ya raia wake wanaondoka nchini humo na kukamatwa katika mataifa mengine Tanzania ikiwemo.

Prof. Kabudi amesema Mpaka sasa takribani raia zaidi ya 1,300 wanashikiliwa katika magereza mbalimbali nchini Tanzania huku idadi ya wanaoendelea kukamatwa ikiongezeka jambo linalosababisha mrundikano wa wafungwa katika magereza ya nchi hiyo.

Ameongeza kuwa katika mazungumzo hayo Tanzania na Ethiopia zimekubaliana kuchukua hatua za pamoja zitakazowezesha kurejeshwa wafungwa na wahamiaji haramu wan chi hiyo wanaoshikliwa Tanzania kwa utaratibu utakaokubalika baada ya majadiliano ya kina na kitaalamu.

Akizungumza kupitia kwa msemaji Waziri wa mambo ya Nje wa Ethiopia Dkt. Workneh Gebeyehu amekiri kuwepo kwa tatizo la vijana wan chi yake kuondoka nchini humo kinyume cha utaratibu na kuitumia Tanzania kama mapito wakielekea katika nchi za kusini mwa Afrika na Ulaya na kuongeza kuwa serikali ya nchi hiyo itachukua hatua madhubuti kukabiliana na hali hiyo.

Pia ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano wake katika suala la wahamiaji haramu kwa kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu raia wa Ethiopia wanaoshikiliwa Tanzania na kwamba wana imani kuwa mazungumzo yatakayofanyika yatasaidia kuwarejesha raia hao nchini Ethiopia kwa njia ya pamoja watakayokubaliana.

Kando na masuala hayo ya wahamiaji haramu pia Prof. Kabudi na Dkt. Workneh wamezungumzia masuala mbalimbali ya mashirikiano baina ya Tanzania na Ethiopia ikiwa ni pmaoja na mashirikiano katika masuala ya anga,miundombinu na ubadilishanaji wa utaalamu kuhusu ujenzi wa mabwawa ya umeme ili kuziwezesha nchi hizo kupiga hatua za kimaendeleo katika nyanja ya Uchumi.