**************************
NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
TAKUKURU Mkoani Pwani, imetoa rai kwa viongozi wa kuchaguliwa wakiwemo madiwani na wabunge kurudi kwa wananchi na kwenda kujitathmini kuwaeleza juu ya utekelezaji wa ahadi na mambo waliowafanyia katika kipindi cha uongozi wao ili wachaguliwe kwa haki badala ya kujiingiza kwenye dimbwi la utoaji rushwa wakati wa uchaguzi mkuu.
Aidha imewataka madiwani kufuatilia na kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao na endapo watabaini shaka yoyote watoe taarifa TAKUKURU kwa msaada zaidi.
Akitoa tahadhali za kiuchaguzi wakati wa kikao cha baraza la madiwani ,Kibaha Mjini, mwakilishi kutoka TAKUKURU Pwani, Juma Swalehe alisema ,kila kiongozi wa kuchaguliwa atavuna kwa alichokipanda ndani ya miaka mitano ya uongozi wake.
Alieleza kwamba, ifikie hatua ya kubadili mtizamo wa kushinda uongozi kwa fedha ama kutoa rushwa ya vitu bali wajipime kwa yale waliyoyaahidi kwa wananchi na kueleza walichotekeleza na nini serikali imefanyia wananchi wake.
“Elimu tumeshatoa mara kwa mara ,kuanzia sasa nendeni kwa wananchi wenu mkajieleze mlichowafanyia,:wawapime mapema kabla ya uchaguzi ili kama mnaweka nia tena iwe rahisi kwenu wakati wa kampeni na uchaguzi”alifafanua Swalehe.
Pamoja na hilo Swalehe ,alimuelekeza mkurugenzi,mwenyekiti wa halmashauri kuunda kamati za kudhibiti uadilifu pia mmomonyoko wa maadili kwa watumishi .
Nao baadhi ya madiwani akiwemo diwani wa viti maalum Selina Wilson ,alielezea, hata mh.Rais John Magufuli serikali yake inapiga vita masuala ya rushwa na inahitaji utawala bora hivyo viongozi wa kuchaguliwa wanapaswa kuwa sehemu ya kuunga mkono juhudi hizo.
Diwani wa kata ya Tumbi, Hemed Chanyika alifafanua kuwa, ndani ya Chama Cha Mapinduzi imeshaelekezwa ,kiongozi akiwa na chembe ya rushwa hafai kuongoza jamii na ni vyema aenguliwe mapema kabla ya uchaguzi.
“Na hao TAKUKURU wasiwe miongoni mwa watu wanaochukua rushwa kwa siri ili kusaidia kurudi kwa hao mabebari wanaowasema bali waweke msimamo wa dhati kushirikiana na serikali kupiga vita rushwa ya uchaguzi”alisisitiza Chanyika.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Mailmoja ,Ramadhani Lutambi aliwataka wananchi nao wasiwaendekeze viongozi wanaopitapita kuwapa rushwa ili kuwachagua kwani endapo wakiwa na msimamo hakuna kiongozi atakae warubuni kwa kuwapa rushwa.
Aliishauri TAKUKURU kuharakisha kufanyia kazi mashauri yanayopatikana yasikae mezani kwa kipindi kirefu na washuke ngazi za chini na kata ili kufanya kazi na jamii.