Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amefanya ziara ya kukagua ukarabati wa miundombinu ya shule ya wasichana ya sekondari Msalato uliofanywa na wizara katika shule hiyo pamoja na kuzungumza na wanafunzi wa hiyo.
Baada ya kukagua ukarabati huo Waziri Ndalichako alizungumza na walimu, watumishi na wanafunzi wa shule hiyo na kuwataka kuendelea na juhudi wanazozifanya katika kuhakikisha shule hiuyo inakuwa na matokeo mazuri kama ilivyofanya kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo ya kuongeza ufaulu na kutopata daraja la sifuri katika matokeo ya kidato cha nne.
“Nawapongeza kwa kuwa shule ya wasichana yenye matokeo mazuri kwa kipindi kirefu, niwaombe ongezeni bidii ili matokeo ya elimu bila malipo yaweze kuonekana kwani rais anapambana kuhakikisha elimu inakuwa bora ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti ya Elimu sekondari kwa asilimia 70 mwaka uliopita” amesisitiza Profesa Ndalichako.
Waziri Ndalichako ameeleza kuwa matokeo chanya ya Sera ya Elimu Bila Malipo ni kuongezeka wa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na kutakiwa kujiunga na kidato cha kwanza, ambapo ameeleza kuwa takwimu zinaonesha kuna ongezeko la wanafunzi hao kutoka 366,296 mwaka 2016, kufikia 680,000 mwaka 2020, na inatarajiwa Mwaka 2023 watakuwa 1,400,00 na hivyo kuhitajika kuongeza miundo mbinu ya shule za sekondari kwa zaidi ya asilimia 100.
Ndalichako amesema ni katika kuangalia hili Serikali ilikuja na Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) na kuomba ufadhili wa Benki ya Dunia. Ndalichako amesema kuwa anaamini Benki ya Dunia itaridhia na kupitisha mradi huo muhimu kwa taifa kwa sababu unakwenda kutatua mahitaji ya haraka ya kielimu ya watoto wa Kitanzania na kutimiza Malengo Endelevu ya maendeleo.
Waziri Ndalichako amefafanua kuwa kuwa mradi huu una lenga kuongeza idadi ya shule za sekondari ambazo zitajengwa katika maeneo karibu na jamii ili watoto wasoe katika mazingira salama, kuongeza shule za bweni hususan kwa ajili ya watoto wa kike, upanuzi wa shule kongwe 50 ili kuongeza nafasi na kukamilisha maabara. Kimsingi, wanafunzi zaidi ya 6,000,000 wa kike na kiume watanufaika na Mradi katika kipindi cha miaka 5 ijayo.
Mradi pia utawezesha uboreshaji wa vituo vya utoaji elimu kwa Mfumo Mbadala kupitia vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) na Vituo vya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (AEP) Centers na ambao utawezesha wanafunzi awalioacha Shule kwa sababu mbalimbali kupata elimu na kumuwezesha kurejea katika mfumo rasmi.
“ lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa kila mtoto wa kitanzania anapata elimu na katika miaka miwili iliyopita tulifanya kazi kwa pamoja na wadau na kuja na mfumo huu ”
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu Gerald Mweli amesema TAMISEMI itaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknlojia kuhakikisha inakamilisha ukarabati wa shule kongwe kwa kukarabati maeneo ambayo hayakufikiwa katika awamu ya kwanza huku akipongeza juhudi za walimu wa shule hiyo kwa kuondoa daraja sifuri.
Mkuu wa shule Neema Maro ameishukuru serikali kwa namna inavyokarabati shule kongwe ikiwa pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya ufundishaji na ujifunzaji, huku akiomba kutatuliwa changamoto ya uzio, uchakavu wa baadhi ya miundombinu ambayo bado haijakarabatiwa shuleni hapo.