Mratibu wa kifua kikuu na Ukoma Hospitali ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole akitoa elimu juu ya ugonjwa wa kifua kikuu kwa wananchi wa kijiji cha Naikula wilayani humo kabla ya uzinduzi rasmi wa kampeni ya Uelimishaji,uchunguzi na Upimaji wa ugonjwa huo ambayo itafanyika Nyumba kwa nyumba inayolenga kutokomeza kabisa kifua kikuu kabla ya mwaka 2030 katika wilaya hiyo.
Picha na Mpiga Picha Wetu
………………………………………………………………………………………………..
Na Mwandishi Maalum,
Tunduru
HOSPITALI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma imezindua kampeni mpya ya upimaji na uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu kwa mwaka 2020 ijulikanayo nyumba kwa nyumba yenye lengo la kutokomeza ugonjwa huo kabla ya mwaka 2030.
Katika kampeni hiyo, Hospitali ya wilaya imejipanga kuhakikisha kila mwananchi anafanyiwa uchunguzi wa vimelea vya kifua kikuu kama mkakati wake wa kuungana na Shirika la Afya Duniani(WHO) kumaliza kabisa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Akizundua Kampeni hiyo iliyoanza kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na watu wazima katika kijiji cha Naikula, Katibu tawala wa wilaya Ghaib Lingo kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo Julis Mtatiro licha ya kuipongeza Hospitali ya wilaya kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma kwa jitihada zake katika kutokomeza maradhi hayo.
Ameitaka Hospitali ya wilaya na wadau wengine ikiwemo Shirika lisilo la kiserikali la MDH linalofanya kazi na Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya kifua kikuu,ukimwi na Malaria kuongeza mikakati itakayosaidia kuwaibua wananchi wengi zaidi wenye ugonjwa huo ili wapatiwe tiba na waweze na hatimaye waweze kushirikiana na Watanzania wenzao katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Alisema, licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na kitengo cha kifua kikuu, lakini ipo haja ya kuongeza nguvu katika mapambano ya kutokomeza ugonjwa huo kwani bado kuna watu wengi majumbani ambao hawajafikiwa na matibabu na wanaendelea kuteseka na kuangaika kutafuta tiba sahihi ya ugonjwa huo unaotajwa kuwa miongoni mwa magonjwa kumi yanayoogoza kuuwa watu wengi hapa Ulimwenguni.
Aidha, ameitaka jamii kushirikiana na Serikali kuwafichua watu wenye dalili na wanaougua kifua kikuu kwa kuwapeleka Hospitali kufanyiwa vipimo na dawa badala ya kuwaficha majumbani.
Sambamba na hilo, amewaomba Watanzania kuendelea na utamaduni wao wa upendo na kuwapa ushirikiano watu wanaougua ugonjwa huo ili wapate faraja badala ya kuwatenga, kwani mgonjwa aliyeanza kutumia dawa hakuna uwezekano wa kuambukiza mtu mwingine.
Alisema,siku za nyuma jamii ilikuwa na kasumba mbaya ya kuwatenga wagonjwa wa kifua kikuu wasichanganyike na jamii ili kuepuka uwezekano wa kuambukiza watu wengine, jambo ambalo kwa sasa halipo hasa baada ya serikali na wadau wengine kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Lingo alisema, serikali ya wilaya itahakikisha inatoa ushirikiano katika kampeni dhidi ya ugonjwa huo kwa kutoa vifaa ikiwemo magari na mahitaji mengine pale itakapohitajika ili kufanikisha kampeni hiyo muhimu kwa wananchi wa Tunduru.
Aliwaeleza wananchi waliofika katika uzinduzi huo kuwa, serikali itahakikisha inasimamia matibabu ya watoto wote na hata watu wazima wakaobainika kuugua kifua kikuu na kuwaonya wazazi ambao watawakatisha dawa watoto wao.
Hata hivyo katika uzinduzi huo,Lingo alibaini kuwepo baadhi ya changamoto mbalimbali ikiwemo uwajibikaji mdogo wa wazazi katika malezi ya watoto wao, na kueleza kuwa ndiyo sababu mojawapo iliyochangia kuongezeka kwa maradhi ya kifua kikuu hasa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Katika hatua nyingine, katibu tawala hakuridhishwa na mahudhurio ya wananchi hususani wanaume ambapo amewaagiza viongozi wa vijiji na kata kuhakikisha wanafikisha ujumbe kwa jamii yote kila kampeni hiyo itakapofanyika katika vijiji mbalimbali.
Kwa upande wake,Mratibu wa kifua kikuu na Ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema, kampeni ya uchunguzi ya vimelea vya kifua kikuu mwaka huu inalenga kuwaibua wagonjwa 768 ambao watapatikana kupitia zahanati,vituo vya Afya, Hospitali na kwa wahudumu wa Afya ngazi ya jamii.
Alisema, malengo ya wizara ya Afya kuhakikisha kampeni ya uelimishaji, uibuaji na uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa huo inawafikia wananchi wote ikiwemo makundi maalum ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na watu wazima.
Dkt Mkasange alisema, kampeni ya mwaka huu ni tofauti na ile ya siku za nyuma kwani inafanyika nyumba hadi nyumba na hakuna mwananchi atakayeachwa.
Kwa mujibu wa Kihongole,Hospitali ya wilaya kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma imedhamiria kuwafikia wananchi wote wale wanaoishi mjini na vijijini kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi ambao utawezesha wananchi kujua hali za Afya zao na wale watakaobainika wataanzishiwa dawa.
Alisema, kwa kawaida kifua kikuu ni ugonjwa ambao unaambukiza kwa njia ya hewa ambapo mtu mwenye ugonjwa huo anapokohoa bila kuziba mdogo ni rahisi kuambikiza mwingine aliye karibu.
Mkasange alitaja dalili kwa mtoto mdogo aliyeambukizwa ugonjwa huo ni kupungua uzito,kukosa raha,kuchelewa kukua,kulia lia kukohoa zaidi ya wiki mbili na kwa mtu mzima ni pamoja na kukohoa damu na kutokwa na jasho hasa nyakati za usiku.
Alisema,mwaka 2019 lengo ilikuwa kuwagundua wagonjwa 641 lakini waliweza kuwagundua wagonjwa 591 sawa na asilimia 92, kati yao wagonjwa 18 walipoteza maisha.
Waliopima virusi vya ukimwi ni 591 sawa na asilimia 100 ambapo waliokutwa na virusi walikuwa 80 sawa na asilimia 13.5, na walioanzishiwa dawa za kufubaza makali ya virusi ni 76.
Aidha alieleza, watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na tano ni asilimia 13.5 na kati ya wagonjwa wote 591 ambao wamepatikana kwa jitihada za makundi yanayoibua wagonjwa katika jamii mia tano sawa na asilimia 84.6.
Hata hivyo,Dkt Kihongole ameiomba Ofisi ya Mkuu wa wilaya kushirikiana na kitengo cha kifua kikuu katika kampeni hiyo na mkakati mzima wa kuwaibua wananchi wenye vimelea vya ugonjwa huo ambao matibabu yake yanatolewa bure katika zahanati,vituo vya Afya na Hospitali zote hapa nchini ili wapate tiba sahihi.
Mwakilishi wa shirika la MDH linalofanya kazi na Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya kifua kikuu Dkt Nixson John alisema, katika mkoa wa Ruvuma wilaya ya Tunduru ni miongoni mwa Wilaya zinazoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wenye kifua kikuu,ndiyo maana MDH kwa kushirikiana na Hospitali ya wilaya Tunduru inapita kila kijiji kwa ajili ya uelimishaji na upimaji vimelea vya ugonjwa huo.
Alisema, katika kampeni hiyo wana washirikisha Waganga wa Tiba asili na tiba mbadala ambao wana jukumu la kuwahisi wateja wenye Kifua Kikuu miongoni mwa wateja wao kwenye vilinge na kuwashirikisha Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii kwa ajili ya kukusanya sampuli za makohozi na kupeleka Hospitali ya wilaya kwa ajili ya uchunguzi na wale wanaobainika wanaanzishiwa dawa.
Kwa mujibu wa Dkt Nixon alisema wilaya ya Tunduru ina jumla ya wahudumu wa Kifua Kikuu 30, Waganga wa Tiba asili wanaojihusisha na Kifua Kikuu 5, na Pikipiki za kusafirisha sampuli za makohozi 2.
Alisema, katika ushirikishaji wa waganga hao kuna mafanikio makubwa yaliyopatikana kwani mwaka 2019 jumla ya watu 8 walibainika kuwa na kifua kikuu kupitia kwa waganga hao.