Nabii Joshua akizungumza na vyombo vya habari kuelezea kuhusu uzinduzi wa Programu ya Kitaifa la Kuliombea Taifa.
**************************
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Programu ya Kitaifa ya Kuliombea Taifa inayoratibiwa na Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania.
Programu hiyo ya kitaifa ambayo itaratibiwa nchini kote kupitia kusanyiko kubwa la ibada itakuwa inalenga kuombea Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli na wasaidizi wake ili Mungu azidi kuwapa hekima, maarifa na bidii ya kuendelea kuwahudumia Watanzania.
Hayo yalisemwa jana na Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania na Mratibu wa Programu hiyo kitaifa, Nabii Joshua Aram Mwantyala wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.
Alisema kuwa, uzinduzi huo utafanyika Februari 15 na 16, mwaka huu katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo katika Chuo cha Mipango jijini Dodoma.
“Tunatarajia hii itakuwa ni programu ya kipekee sana, maana Mungu anaenda kuonekana katika Taifa letu, tumekuwa katika maombi mfululizo kwa ajili ya kuombea uzinduzi huo ambao itakuwa ni ibada ya miujiza na uponyaji.
“Hivyo, nichukue nafasi hii kuwakaribisha Watanzania wote katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Chuo cha Mipango jijini Dodoma, Februari 15 hadi 16, mwaka huu, tuamke Watanzania, tuliombee Taifa,”alifafanua Nabii Joshua.
Alisema, baada ya uzinduzi huo programu hiyo itazunguka mikoa yote nchini kwa ajili ya kufanya maombi, hatua ambayo itasaidia miradi na mipango inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano ikafanikiwe kwa haraka, kwa kuwa wataikabidhi mbele za Mungu.
Nabii Joshua alifafanua kuwa, wito huo wa kuliombea Taifa ni kwa Watanzania wote, hivyo bila kujali imani, kabila au rangi kila mmoja atashiriki kwa ajili ya kumlilia Mungu ili azidi kulitendea mema Taifa letu.
“Kwa sababu tulimlilia akatupatia kiongozi na Rais Dkt.Magufuli ambaye anatutetea wanyonge na kuzipigania rasilimali zetu ili ziweze kutumika katika uwiano sahihi kwa maslahi ya Watanzania wote, vivyo hivyo tunapaswa kumuombea Rais wetu ili kwa kushirikiana na wasaidizi wake wazidi kuliletea Taifa letu heshima kubwa, hakika Mungu ameweka kusudi ndani yao kwa maslahi ya Taifa, tunaamini yote yanawezekana,”alifafanua Nabii Joshua.
Kiongozi huyo alisema, katika maombi hayo watamuomba Mungu azidi kuibariki miradi yote iliyopo nchini ikiwemo ya kimkakati kuanzia barabara, reli, viwanja vya ndege, elimu, afya, nishati, mipango ya kudumisha amani na upendo, uchaguzi ujao na mingine mingi.