Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imepongezwa na wananchi mkoani Manyara kwa kufanya tafiti zinazolenga kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Pongezi hizo zimetolewa mwishoni mwa wiki katika mahojiano maalum na wananchi wa Dareda mkoani Manyara ambako Utafiti wa Feed the Future unaendelea kufanyika.
Bw. Patrice Martin Ami mkaazi wa Dareda mkoani humo amesema utafiti huo utaiwezesha Serikali kubaini hali halisi ya maisha ya wananchi wake na hivyo kuchukua hatua stahiki kulingana na matokeo ya utafiti huo yatakapotolewa.
“Tunaamini kuwa utafiti huu unafanyika kwa maslahi ya wananchi na utawezesha wananchi kupiga hatua baada ya kukamilika kwake kwa kuonesha hali halisi katika masuala yote yanayofanyiwa utafiti” alisisitiza Ami.
Utafiti wa Feed the Future ambao unaangalia hali ya ustawi katika kaya ikiwemo upatikanaji wa chakula, aina ya milo katika kaya kwa wanawake, huduma za afya, udumavu kwa watoto na nafasi ya mwanamke katika kufanya maamuzi unafanyika katika mikoa Dodoma, Iringa, Manyara, Mbeya, Morogoro pamoja na mikoa ya Zanzibar.
Bwana Ami alimueleza mwandishi wetu kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejikita katika kuhakikisha kuwa inawaletea wananchi maendeleo katika nyanza zote hivyo utafiti huo ni sehemu ya nyenzo muhimu kwa Taifa lolote kufikia maendeleo.
Kwa upande wake, Mkazi wa mwingine wa Dareda, Bw. James Sebastian amesema kuwa utafiti huo utasaidia kuongeza kasi ya maendeleo katika maeneo yao baada ya ripoti ya mwisho kutolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Aidha, utafiti huo utakapokamilika unatarajiwa kuwa kichocheo cha maendeleo katika maeneo yote yatakayohusika.
Utafiti huo unafadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la nchi hiyo (USAID) na kutekelezwa kwa pamoja na Benki ya Dunia na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.