……………………………………………….
Alex Sonna, Dodoma
WAKALA wa Vipimo Tanzania(WMA) imetoa semina kwa wabunge wa Kamati ya Bunge ya viwanda, biashara na mazingira, huku ukieleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk.John Magufuli.
Akizungumza kuhusu semina hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Dk. Ludovick Manege, amesema semina hiyo imelenga kuwaelimisha wabunge wa kamati hiyo kuhusu majukumu ya wakala huo na mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka minne.
Amesema jukumu lao ni kumlinda mlaji katika vipimo vinavyofanyika, na matumizi ya vipimo yawe sahihi, ili mnunuaji wa bidhaa apate stahiki ya kipimo sahihi, na serikali kupata mapato sahihi.
“Tuna changamoto ambazo tunaziona kwetu ni fursa, kwa mfano mabadiliko ya teknolojia, uchache wa watumishi, Wakala lazima ijipange kupima bidhaa zote viwandani ili zinapoingia sokoni ziwe kwenye vipimo sahihi,”amesema.
Akizungumzia kuhusu mafanikio, Afisa huyo amesema mafanikio hayo ni pamoja na kukamilisha kwa kituo kikubwa cha kupima malori ya mafuta kilichopo Kibaha.
“Tulikuwa na kituo chetu Ilala ambacho kilikuwa kinapima magari mawili hadi matatu, lakini kwasasa kilichopo kinapima magari 70,”amesema
Pia amesema wamefanikiwa kufanya uhakiki kwenye madini kwa kuhakikisha mizani yote inayotumika ni sahihi ili serikali ipate mapato sahihi bila udanganyifu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo,Suleiman Saddiq, ameshauri WMA, kuweka mkazo zaidi katika vituo vya mafuta kutokana na baadhi kufanya udanganyifu wa vipimo hususan siku za jumamosi na jumapili.
Amesema kuna tatizo kwenye vituo vya mafuta kutokana na baadhi kufanya udanganyifu vipimo na kuwaibia wateja siku za jumamosi na jumapili.
Ameomba eneo hilo liwekewe mkazo ili wanaofanya vitendo hivyo wachukuliwe hatua bila kuoneana aibu na vituo vinavyorudia makosa hayo vipewe adhabu kali zaidi ili watanzania wasiendelee kuibiwa.
“Tunaomba wakala waendelee na jitihada wanazofanya, wametueleza matatizo yao na sisi kama kamati tumechukua tutapeleka ndani ya bunge ili kuishauri serikali kama vile suala la rasilimali watu,”alisema.
Naye, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, amesema ushauri walioutoa wabunge, wizara imechukua ili kufanya maboresho na wakala utatue kero zinazowakabili watanzania.
Amesisitiza WMA kutoa elimu na kuagiza taasisi zote zinazotoa huduma kwa watanzania kutoa elimu kwa kina ili kuondoa kero kwa wananchi.