Waziri wa maji Profesa Makame Mbarawa kulia,akimuelekeza jambo meneja wa wakala wa maji(RUWASA)wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Mhandisi Samwel Sanya wakati alipotembelea mradi wa maji Lilambo ambao ujenzi wake unasuasua kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wa mkandarasi wake Kampuni ya PNR Services Ltd ya Dar es slaam ambayo imeshindwa kukamilisha mradi huo kwa wakati,
Picha na Mpiga Picha Wetu,
****************************
Na Mwandishi Wetu,
Songea
WANANCHI wa kata ya Lilambo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,wamemlalamikia mkandarasi anayejenga mradi wa maji Kampuni ya PNR Services Ltd kuchelewesha mradi huo hali inayosababisha waendelee kutumia maji ya visima vya asili ambavyo sio safi na salama.
Wakitoa kilio chao mbele ya Waziri wa maji Profesa Makame Mbarawa walisema, serikali ilipeleka mradi wa maji katika kata hiyo tangu mwaka 2017 lakini jambo la kusikitisha bado haujakamilika na kila wanapomfuata mkandarasi ili kufahamu sababu za kusua sua wanapata majibu yasio ridhisha kutoka kwa mkandarasi.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Filbert Millanzi alimweleza Waziri Mbarawa kuwa, wananchi wa kata ya Lilambo hawajawahi kufikiwa na huduma ya maji ya bomba tangu Nchi ipate uhuru mwaka 1961 badala yake wamekuwa wakishuhudia wananchi wa maeneo mengine ya Tanzania wakila matunda ya Serikali yao kwa kupata maji.
Aidha,ameiomba wizara ya maji kuwa na huruma kwa wananchi wa kata hiyo kukamilisha mradi huo ambao ni dhahiri mkandarasi wake ameonekana kushindwa kukamilisha mradi huo ili wananchi wapate maji.
Millanzi ambaye ni Mwalimu mstaafu alisema, tatizo la mradi huo kutokamailika kwa wakati ni uwezo mdogo wa mkandarasi,kwani hata vibarua walioshiriki kuchimba mitaro na kufanya kazi nyingine wameacha kwa sababu hawajalipwa stahiki zao tangu mwaka 2017.
Diwani wa kata ya Lilambo Yob Mapunda alisema, mradi huo ulianza mwaka 2017 na ulitakiwa kukamilika tangu mwaka 2018 lakini hadi sasa bado haujaka,milika na Serikali ilishakatisha mkataba hata hivyo mkandarasi alikwenda mahakama ya Usuluhishi ambapo alishinda kesi na kumrudisha kuendelea na kazi.
Lakini licha ya kurudishwa,bado hakuna kazi yoyote iliyofanyika katika mradi huo na badala yake mkandarasi huy haonekani kabisa eneo la mradi jambo linalotia shaka kama mradi utakamilika na wananchi kupata maji safi na salama kwa matumizi yao ya kila siku.
Alisema, serikali ilipopeleka mradi huo mwaka 2017 wananchi wa Lilambo walikuwa na matumaini makubwa ya kuondokana na kero ya maji,lakini furaha yao imekwisha baada ya kuona hakuna juhudi zinazofanyika katika mradi huo.
Mapunda alisema, mradi huo kwa sasa sio rafiki kabisa kwani umekuwa chanzo cha ugomvi kati ya wananchi ambao wanawatuhumu viongozi akiwemo diwani kuwa wanahusika kukwama kwa mradi kwa kile walichodai kugawana na mkandarasi fedha za mradi huo.
Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema, ameunga mkono uamuzi wa wizara ya maji wa kuwatumia wataalam wa wizara hiyo kutekeleza miradi ya maji badala ya kuendelea na wakanadarasi kwani hatua hiyo itasaidia kuokoa fedha nyingi ambazo zilikuwa zinatumika vibaya na wakandarasi kwa kushirikiana na baadhi ya wahandisi wa maji kuiba fedha za umma.
Meneja wa wakala wa maji Ruwasa wilaya ya Songea Samwel Sanya alisema, mradi wa maji Lilambo ulianza kutekelezwa mwaka 2017 na unatakiwa kukamilika mwezi Machi mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni 1.4,hata hivyo kutokana na kasi ndogo ya utekelezaji wake hakuna dalilil ya kukamilika.
Waziri wa maji Profesa Makame Mbarawa alisema, mkandarasi huo ni mbovu na hakustahili kupewa mradi wa maji Lilambo kwani licha ya kukosa mtaji wa fedha pia gharama za mradi ni kubwa ikilinganisha na miradi mingine ya maji.
Profesa Mbarawa, amekataa kumlipa mkandarasi sehemu ya fedha hadi atakapoweka dhamana ya asilimia kumi na tano ya gharama ya mradi ambayo ni sawa na shilingi milioni 110 ili alipwe milioni 170 na hatua hiyo inalenga kuepusha udanganyifu unaoweza kufanywa kwa mkandarasi kuchukua fedha na kukimbia na kuwaacha wananchi wakiangaika na kero ya maji.
Aidha,amemuagiza meneja wa Ruwasa wilaya ya Songea kumsimamia mkandarasi huyo ili aweze kukamilisha kazi, sambamba na kumtaka Meneja wa Ruwasa mkoa wa Ruvuma Mhandisi Patrick Hans kuhakikisha ananunua mabomba na baadhi ya vifaa vya mradi kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo ili kuepusha udanganyifu unaoweza kufanywa na mkandarasi.
Profesa Mbarawa aliwaeleza wananchi kuwa,tatizo kubwa lililokwamisha kukamilika kwa mradi huo ni viongozi waliokuwepo wakati huo kushindwa kusimamia fedha na miradi ya maji badala yake, walishirikiana na wakandarasi kuhujumu fedha hivyo kusababisha kata ya Lilambo na maeneo mengine ya mkoa wa Ruvuma kukosa maji safi na salama.
Alisema, wananchi wa Lilambo wana haki ya kupata huduma ya maji kama ilivyo katika maeneo mengine ya nchi ambapo alisisitiza kuwa, Serikali ya awamu ya tano itahakikisha mradi huo unakamilika na wananchi wanapata huduma ya maji.