Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania leo imetangaza kufunga huduma kwa Wateja wake 157,000 ambao wameshindwa kujisajili kwa kutumia alama za vidole.
Hatua hii inafuatia agizo la Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kuyaagiza makampuni yote ya Simu nchini kuwafungia wateja ambao wameshindwa kusajili kwa kutumia alama za vidole (biometria) ifikapo Januari 20, 2020.
Akitangaza uamuzi huo leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC Hisham Hendi, amewaomba Wateja wote waliofungiwa laini zao kutembelea vituo vya huduma au mawakala wa kampuni hiyo zaidi ya 35,000 nchini kusaijili laini zao ili kuendelea kufurahia huduma za kampuni hiyo.
“Baadhi ya maduka yetu kwenye miji mikubwa yatakuwa wazi masaa 24 siku saba za wiki, ili kuhakikisha kwamba wateja wetu wote ambao wana vitambulisho vya Taifa wanasajiliwa na hivyo kuendelea kupata huduma za kampuni yetu ikiwa ni pamoja na huduma za M-Pesa,” alisema Hendi.
Aliongeza kwamba Wateja walioathiriwa na zoezi hili ni wale tu waliopokea namba za vitambulisho vya Taifa kutoka mamlaka ya vitambulisho hivyo (NIDA), lakini wameshindwa kujisajili kwa sababu moja au nyingine, “kwa kuwa zoezi hili ni endelevu, wateja wetu wote ambao hawajapata namba za utambulisho kutoka NIDA, waendelee na mchakato wa kupata namba hizo au vitambulisho vitakavyowawezesha kujisajili kwa kutumia alama za vidole na kuepuka usumbufu wa kufungiwa huduma.”
“Tukiwa ni kampuni iliyo orodheshwa kwenye soko la hisa nchini, tuna jukumu la kufuata sheria na taratibu zote zilizowekwa na serikali pamoja na vyombo vilivyo chini yake,” alisema Mkurugenzi.
Hendi aliongeza kwamba zoezi la usajili kwa alama za vidole litasaidia kupunguza idadi ya matapeli wanaosumbua wateja, “kusajili kwa biometria unatuhakikishia kwamba kila mmoja aliyesajili anajulikana kwa kutumia alama hizo, hii itarahisisha vyombo vya usalama kupambana na matukio hayo ya kitapeli,” alifafanua Hendi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja, Bi Harriet Lwakatare alisema “Wateja wanaweza kubofya namba *152*00# au kutuma ujumbe mfupi kwenda namba 15096 ili kupata namba za vitambulisho vyao ambazo watazitumia kujisajili kwa alama za vidole. Kwa wale walioathiriwa na zoezi hili la kufungiwa wasiwe na wasiwasi kwa vile taarifa zao zitatunzwa kwa muda wa miezi sita ambapo wanatarajiwa wawe wamejisajili kwa alama za vidole.”
“Wateja wote waliofungiwa wanaweza kupata huduma zetu za kidijitali kupitia mitandao ya kijamii kupata taarifa za namna ya kuendelea au kukamilisha usajili,” alimalizia Bi Lwakatare.
Mwanzoni mwa mwaka jana, serikali kupitia mamlaka ya mawasiliano nchini ilitoa maelekezo kwamba wamiliki wote wa laini za simu wasajiliwe upya kwa kutumia biometria (biometric registration), usajili kwa alama za vidole unatumiwa kama namna ya “kumjua mteja wako” [Know Your Customer (KYC)] na kudhibiti matapeli wanaotumia mitandao ya simu kutapeli watumiaji wa huduma za mawasiliano.