Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.Subira Mgalu (kushoto) akipungia wananchi mara baada ya kuhutubia kwenye Kijiji cha Kibindu Jimbo la Chalinze mkoani Pwani Januari 21, 2020.
Na mwandishi wetu, CHALINZE.
NAIBU Waziri wa Nishati Mhe.Subira Mgalu amesema debe tatu za mahindi au kuku tatu zinatosha kuweka umeme ndani ya nyumba.
Mhe.Mgalu ameyasema hayo leo Januari 21, 2020 wakati akizungumza na wanakijiji wa Kibindu Jimbo la Chalinze Mkoani Pwani wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya kupeleka umeme vijiji vya Kibindu na Talawanda jimbo la Chalinze mkoani Pwani.
“Serikali ya awamu ya Tano chini ya uongozi wake Rais Dkt.John Pombe Magufuli imedhamiria kufikisha umeme kila kijiji ifikapo Juni 2020.
“Serikali imeshusha gharama za kuweka kutoka bei ya awali hadi shilingi elfu 27,000/-“. Alisema Naibu Waziri Mgalu.
Ameipongeza TANESCO na REA kwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo wa kupeleka umeme kwenye vijiji hivyo ambapo kwa Kijiji cha Kibindu mradi unatekelezwa kwa umbali wa kilomita 60 wakati kijiji cha Talawanda ni kilomita 26.
“Umeme huu hauchagui nyumba ya nyasi, tope au tofali, zote zinastahili kuwekewa umeme na tunawasihi wananchi mtumie umeme.” Alisisitiza Mhe. Naibu Waziri.