Na Munir Shemweta, WANMM KIGOMA
Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Kigoma limekusanya kiasi cha shilingi 618,246,592 sawa na asilimia 70 ya makusanyo ya mwaka ambapo matarajio ya shirika hilo ilikuwa kukusanya asilimia 50 kufikia Desemba 2019.
Akitoa taarifa ya makusanyo ya kodi kwa miradi ya Shirika lake kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kwa mwaka 2019/2020 wakati wa ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi kwenye mkoa wa Kigoma jana, Kaimu Meneja wa NHC mkoa wa Kigoma Ramadhani Sadick alisema Shirika hilo ilipangiwa kukusanya 886,732,105 na kubainisha kuwa ziada iliyopatikana ilitokana na mahusiano mazuri na wateja wake pamoja na huduma bora zinazotolewa.
Kwa mujibu wa Sadick, Shirika la NHC limekuwa likifanya jitihada za dhati kuhakikisha linaboresha mahusiano na wapangaji ili kuhakikisha panakuwepo maridhiano kati ya shirika na wateja wake jambo alilolieleza linasaidia kupunguza migogoro baina ya pande hizo hasa kipindi ambacho ilipaji kodi ulikuwa ukisuasua.
‘’Shirika limekuwa lifanya mazungumzo na wateja ili kuona namna bora ya kuwasaidia kutekeleza majukumu ya kiupangaji ilhali wakiendelea na biashara zao na tunatoa fursa ya kulipa kodi kwa awamu tofauti na utaratibu uliozoeleka wa kulipa kodi kwa mara moja’’ alisema Sadick.
Akielezea hali ya soko, Kaimu Meneja wa NHC mkoa wa Kigoma, alisema Shirika lake limekuwa likifanya tafiti mara kwa mara ili kuhakikisha bei inazotoza kwenye nyumba za kupanga zinaendana na hali ya soko pamoja na mazingira halisi ya soko la nyumba.
Akigeukia nyumba za kuuza katika mradi wa Mlole, Kaimu Meneja huyo wa NHC mkoa wa Kigoma alisema, Shirika lilijenga nyumba 36 za makazi na nyumba 26 kati ya hizo ziliuzwa huku nyumba 13 zikipangishwa kwa wateja ambao walipewa fursa ya kununua nyumba hizo pale watakapohitaji.
Aidha, alibainisha kuwa, fursa hiyo inatolewa pia kwa mwananchi yeyote anayetaka kununua nyumba zilizopangishwa ambapo mkataba wa upangishaji unatoa fursa kwa mnunuzi asiye mpangaji kununua nyumba yoyote aitakaye.
Kwa upande wale Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amelitaka shirika la nyumba la taifa mkoa wa kigoma kuangalia namna bora ya kushirikiana na halmashauri zilizopo nje ya miji katika kujenga nyumba za watimishi badala ya kuangalia halnashauri za mjini pekee.
Alisema, katika kuhakikisha Shirika la Nyumba linajenga nyumba za bei nafuu kwa watumishi katika halmashauri mbalimbali nchini Naibu Waziri Mabula alitaka shirika hilo kukabidhiwa viwanja huku kazi ya kuweka miundombinu na gharama nyingine ikibaki halmashauri husika.
Aidha, amelitaka shirika la nyumba la Taifa kujenga nyumba kwa kuingia makubaliano na halmashauri kulingana na mahitaji au aina ya nyumba inazohitaji ili kuepuka ujenzi wa nyumba zitakazokosa wanunuzi.